Simulizi : Penzi La Mfungwa Sehemu Ya Kwanza (1)

IMEANDIKWA NA : ALEXIS WAMILLAZO

*********************************************************************************


 Ilikuwa muda wa saa nane usiku zilisikika sauti za wanakijiji wakipiga mayowe.."mwizi mwizii mwizii..", sauti hizo zilitambaa kwa kasi ya ajabu usiku ule kitendo ambacho kiliwafanya wanakijiji waliokuwa wamelala wakaamka ili kumkimbiza mwizi huyo ambaye kimuonekano alionekana kuwa shapu na kasi ya ajabu,alifanikiwa kuruka vigingi mbali mbali akatoka kijijini akakimbilia nje ya kijiji akatokomea kunako mashamba yaliyokuwa kando ya kijiji hicho. Hapo mwizi huyo akawa amefanikiwa kuwatoka hao wanakijiji walioonekana kuwa na hasira kali kwani baada kutokemea nje ya kijiji,walibaki kujilaumu huku kila mmoja akiwa na hamu ya kumkata ili wamuadabishe jambo ambalo lilienda kinyume na malengo yao. Mwizi aliwapotea. Baada mwizi kufanikiwa kuwatoka,wanakijiji waliamua kurudi majumbani kwao. Kesho yake asubuhi palipo pambazuka mwenyekiti wa kijiji alimtaka mjumbe wake apige mbiyu kuitisha mkutano wa kijiji kwa maana siku hiyo palikuwa na agenda mbali mbali alizotaka kusema na wanakijiji hasa kuhusu suala hilo la wizi kushamili kijijini kwake,lakini wakati mbiyu hiyo inapasa kijiji hapo,upande wa pili alionekana kijana Zabroni akiwa ndani ya nyumba yao ambayo ilikuwa imejengwa na miti ikiparatwa udongo huku juu ikiwa imeezekwa nyasi. Kijana Zabroni alikuwa chumbani akihesabu fedha alizopora kwenye duka la muhindi mmoja hapo kijijini kwao,ila kabla hajafikia tamati akasikia mama yake akimuita ikabidi asitishe zoezi hilo haraka sana akazipiga hatua kutii wito wa mama yake ambaye wakati wote alikuwa ni mtu wa kitandani akiugulia ugonjwa wake wa kupolalazi mwili. "Naam mama", aliitika Zabroni baada kumfikia mama yake. Mama Zabroni alipomuona mwanaye kafika, alimtazama kisha akasema "Zabro mwanangu,mimi mama yako tayari nimesha jihakikishia umauti. Huna sababu ya kuendelea kuiba mali za watu ili kuokoa maisha yangu. Tafadhali naomba uachane na hiyo shuguli utakufa kingali kijana mwanangu,fanya kazi za kilimo ili upate fedha za matumizi ya kawaida kwani mama yako sio waleo wala wakesho. Sikia mbiyu imelia,na hii ni kutokana na tukio la jana la wizi.. najua niwewe hakuna mwingine mwizi hapa kijijini. Sasa unajua kwenye huo mkutano watakuwekea agenda gani? Za mwizi ni arobaini mwanangu achana na kazi hiyo wizi haufai baba ", alisema mama Zabroni kwa sauti ya chini kabisa, maneno hayo yalimuumiza sana kijana huyo akajikuta akidondosha chozi kwa uchungu. Ila yote kwa yote Zabroni aliamua kukubaliana na matakwa ya mama yake ili apate kumlizisha kulingana na hali tete aliyonayo, kamwe hapendi kumuona mama yake akikereka. "Sawa mama nimekuelewa " alijibu Zabroni kisha akaamka akarudi chumbani kwake kuendelea na zoezi lake la kuhesabu fedha alizoiba usiku wa jana kwanye duka la muhindi kijiji hapo. Alipo zihesabu hizo fedha akakuta ni kiasi cha pesa shilingi laki nane. Hakika alifurahi sana akajikuta akisema"Lakini nane..pesa nyingi sana hizi,mpambanaji haogopi masikini hachoki..nitaendelea kuiba mpaka nitimize pesa ya kumsafirisha mama yangu aende kutibiwa nje ya nchi", kwisha kujisemea hayo akazikusanya fedha hizo akaziweka kwenye mfuko akaingia ufunguni ambapo palikuwa na shimo,huko akawa amezifukia fedha hizo pasipo mtu yoyote kujua zaidi yake yeye. Alipomaliza hilo zoezi alitoka ndani ghafla akakutana uso kwa uso na baba yake mzazi akiwa amelowa umande. Zabroni akamuuliza baba yake "Baba kulikoni mbona umelowa umande asubuhi yote hii?..", mzee huyo hakujimjibu kijana wake zaidi alizama ndani moja kwa moja mpaka chumbani kwake ambapo alipofika akamtazama mkewe kwa jicho la huzuni, akasikitika sana, ndani ya nafsi yake akajiuliza "Hivi nimemkosea nini Mungu?.." swali hilo lake liliambatana na mchirizi wa chozi.baada chozi hilo alijisonya kitendo ambacho kilimfanya mkewe kumgeukia na kisha kusema "Baba Zabroni kulikoni? kuna nini mume wangu?.."http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Loh! mke wangu nahisi kama dunia imenitenga,kila ninalo lifanya haliendi sawa mpaka muda mwingine najikuta namkufuru mungu kwa kunileta duniani"
"Unaamaana gani?..", akiwa na taharuki alihoji mama Zabroni lakini kabla hajamjibu mkewe,mara ghafla nje ya nyumba yake alisikia mtu akabisha hodi. Baba Zabroni alistuka zaidi hofu ilimjaa akamtazama mkewe kisha akasema "Subiri nikamsikilize kwanza huyu mtu, nakuja sasa hivi", alipokwisha kusema hivyo akatii wito. Hofu na woga ulimjaa baada kufika nje akamkuta ni mzee Fungafunga mdeni wake. "Habari yako bwana Ndalo" Fungafunga alimsalimu baba Zabroni. Mzee Ndalo akainamisha uso wake chini,papo hapo swali likamjia kichwani "Nitamueleza nini leo? Muda nilio muahidi kumlipa pesa zake umewadiwa?.." kwisha kujiuliza hilo swali akaitikia salamu ile "Ni salama tu ingawa sio sana"
"Kwanini? Bado mkewe hali tete?.."
"Ndio bwana hata hivyo nafikiria kukopa pesa nyingine kwa mzee Malila ili niweze kumsafirisha kwenda mbali kidogo na hapa. Nimeambiwa kuna mtaalamu mmoja hivi anaweza kunisaidia "
"Sawa lakini yote kwa yote mzee Ndalo nataka pesa yangu.." alisema mzee Fungafunga huku akiwa amekasirika pasipo mfano. Baba Zabloni akastuka kumuona mzee mwenzake akiwa amemkasirikia punde tu. Hapo akajikuta hana la kufanya,pesa ndani hakuwa nazo nawala hakujua kama usiku wa jana mwanae kaiba pesa nyingi ambazo anaweza kulipa hilo deni na nyingine zikabaki. "Doh nitafanya nini mimi?", alijiuliza mzee Ndalo,akamtazama mzee Fungafunga kisha akasema "Mzee mwenzangu kwa leo nimekwama tafadhali njoo kesho basi uhakika upo! Nipo chini ya miguu yako tafadhali ", mzee Ndelo hakuwa mzito kumpigia magoti mzee Fungafunga ili kudhihilisha kile anacho kisema lakini mzee Fungafunga katu hakutaka kuelewa propganda za mzee Ndalo na ndipo alipochomoa kibiriti kutoka kwenye mfuko wa koti lake kukuu akawasha sigara kisha akasema "Sikia we masikini,ulikuja kwa mikono miwili kuomba msaada lakini malipo unasumbua kulipa. Sasa nakupa dakika tano uwe umeleta pesa yangu hapa la sivyo nachoma kibanda chako.." alisema mzee huyo huku akipuliza moshi wa sigara. Mzee Ndalo alishusha pumzi,pesa hana je atafanya nini ilihali mzee Fungafunga hataki kumuelewa? Akaona hakuna namna akiwa katika hali ya unyonge aliingia ndani akakata kamba aliyokuwa akiwekea nguo Zabroni kisha akajinyonga, aliona hana mbinu nyingine ya kujinusuru mbele ya mzee Fungafunga. Nje mzee Fungafunga alibaki kusubiri akidhania kuwa mzee Ndelo ameingia ndani kumchukulia pesa yake. Muda ulisogea mzee Ndalo hatoki ndani, hatimaye mzee Fungafunga ikamjia akili ya ghafla akadhania kwamba huwenda mzee Ndalo kamtoroka kupitia mlango wa uwani na ndipo alipoamua kuchoma nyumba moto ikiwa ndani yumo mzee Ndalo ambae tayari marehemu pia mama Zabroni ambaye ni mgonjwa hajiwezi. Moto ulitembaa kwa kasi kisha mzee Fungafunga akaondoka zake. Punde baada mzee huyo kutokomea muda huo huo Zabroni naye alikuwa njiani akirudi nyumbani baada kutoka kijiweni kusikilizia watu wanazungumziaje wizi uliofanyika usiku wa jana huku mwizi akiwa ni yeye mwenyewe.


Moshi mzito ulioambatana na kipupwe cha aina yake ulipaa angani kwa kasi huku Zabroni naye akizidi kupiga hatua kurudi nyumbani ilihali ndani ya hiyo nyumba inayoteketea kwa moto ilisikika sauti ya mama Zabroni akipiga mayowe kuomba msaada,lakini kulingana na kuugua kwa kipindi kirefu,ilimfanya sauti yake isikike kwa mbali sana kiasi kwamba mtu aliyepo hatua kumi na tano mbele asingeweze kusikia mayowe hayo. Nyumba ilizidi kupamba moto,mama Zabroni akakosa msaada akafa namna hiyo hali ya kuwa mwili wa mzee Ndalo ambaye naye alikuwa ameshajinyonga nao uliungua,kamba ikakatika mwili wake ukazidi kuteketea ukiwa chini. Zabroni alistuka kuona moshi mkali ukitanda angani,moshi huo ukitokea nyumbani kwao. Hali hiyo ilimfanya kohofia usalama wa nyumbani kwao haraka sana alitimua mbio ili ajue kipi kinachoendelea. "Lahaula" alipigwa na butwaa baada kukuta moto ukiishia huku fito zilizoungua nazo zikidondoka chini. Alipagawa,alipasa sauti kumuita mama yake na baba yake lakini harufu ya miili ya wazazi yake iliyoungua ilimfanya Zabroni kuamini kuwa mama yake kaungulia ndani kwani alijua fika kwa hali aliyokuwa nayo mama yake kamwe asingeweza kujinasua kwenye moto huo. Alilia kwa uchungu Zabroni,akajiuliza wapi alipo baba yake? Wakati anajiuliza swali hilo miguu yake ilionyesha kukosa nguvu,usongo wa mawazo wa kifo hicho cha mama yake ulimfanya apoteze fahamu bila kutambua kuwa si mama yake tu aliyefariki bali na baba yake pia.
Wakati tukio hilo linatokea, ghafla anaonekana mzee Maboso akiwa ametokea shamba. Mzee huyo ni jirani wa marehemu mzee Ndelo. Alistushwa na kile alichokiona,Maboso akastaajabu sana kuona nyumba ya mzee mwenzake ikiwa imeteketea kwa moto,haraka sana akatupa jembe na panga chini akasogea jirani zaidi ili aangalie kama kapona mtu hasa hasa mama yake Zabroni ambaye alifahamu fika mama huyo hajiwezi. Lakini kabla hajasogea alimuona Zabroni chini akiwa amepoteza fahamu. Hapo alisitisha kwanza safari yake ya kwenda kujua kama kuna mtu kapona kwenye moto huo akasogea kumuangalia Zabroni, napo alisimama baada kukuta Zabroni kuzimia. Pumzi alishusha Maboso,akiwa na hofu akaendelea kuzipiga hatua za pole pole mpaka mahali ilipo teketea nyumba. "Mungu wangu", mzee Maboso alipagawa baada kuona mwili wa mama Zabroni ukiwa umeungua,alipo tazama upande wa pili akauona mwili wa mzee Ndalo nao ukiwa hivyo hivyo umeungua. Mzee Maboso alisafa,akatazama kulia na kushoto alitimua mbio za kizee kuelekea kwa mwenyekiti wa kijiji kutoa taarifa juu ya maafa yaliyotokea. Alipofika hakumkuta mwenyekiti alimkuta mkewe naye alikuwa akijiandaa kwenda kisimani. Mke wa mwenyekiti alipomuona mzee Maboso kaja hima hima alisimama, kwa mshangao akauliza "Vipi kwema huko?.."
"Hapana sio kwema Siwema", alijibu mzee Maboso huku akihema haraka haraka.
"Mmh inamaana jina la mwanangu hulijui mpaka unitaje jina langu? Hebu tengua kauli yako halafu ueleze kinacho kusibu"
"Sawa, samahani sana. Yote kwa yote Mwenyekiti nimemkuta?.."
"Walaa hapana kaenda kukagulia mashamba yake ila muda sio mrefu atarudi,siunajua leo kuna mkutano wa kijiji? Kunani mzee Maboso? "
"La! Hili ni balaa asikwambie mtu mzee Ndalo na mkewe wamefariki kwa ajari ya moto"
"Mungu wangu weee! Imekuwaje sasa jamani!?.." mke wa mwenyekiti aliuliza huku akisikitika. Mzee Maboso akaishusha pumzi yake kisha akajibu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Doh we acha tu,ukistaajabu ya Musa utayaona ya filauni. Zabroni naye kazimia,yani hata sijui ni kitu gani kimepita kwenye familia ile"
"Sawa acha mimi nikamwambie mjumbe apige mbiyu ya msiba ", aliongeza kusema mzee Maboso na mara moja akaelekea kwa mjumbe kumpa taarifa.
Alimkuta mjumbe akitengeneza baiskeli yake,baada ya salamu akamueleza kila kitu kilichojili. Mjumbe alimtazama mzee Maboso kwa jicho la husda kisha akasema." Kwahiyo nikishatoa taarifa wewe utafaidika nini?..", Maboso alistushwa na maneno hayo aliyoongea Mjumbe.
"Unamaana gani sasa? Mbona sikuelewi!..", akiendelea kumshangaa mzee Maboso alihoji. Mjumbe hakujibu zaidi aliacha zoezi lake la kutengeneza baiskeli akaingia ndani. Punde akatoka na mbuyu mkononi mwake, akaitupa mbele ya mzee Maboso kisha akasema
"Mbiyu hiyo hapo tangaza mwenyewe, toka zamani mimi na mzee Ndalo ni maadai kwahiyo siwezi kupoteza muda wangu mimi" kwisha kusema hivyo akaendelea na kazi yake ya kutengeneza baiskeli. Mzee Maboso alimtazama,akaona hakuna haja ya kumbembeleza akaondoka zake. Ila kabla hajafika mbali,mara ghafla nyumbani kwa mjumbe akaja mzee Fungafunga. Mzee huyo akacheka sana kisha akasema "Mzee mwenzangu wewe ni mwanaume na unamsimamo wa kiume"
"Kwanini bwana" alihoji mjumbe.
"Kukataa kupiga mbiyu hapo upo sawa,Ndalo hafai abadani ", alijibu Fungafunga akimwambia mjumbe,Mjumbe akafurahi sana kupata ujiko kwa mzee Fungafunga asijue Fungafunga ndio muhusika mkuu wa tukio la mauaji ya mzee Ndalo pamoja na mkewe.
Mkutano wa kijiji ulifanyika siku hiyo,waliopata taarifa ya msiba huo walifika na ambao hawakupata hawakufika. Mazishi yalifanywa na wanakijiji wachache sana, hakuna aliyekuwa na taarifa kuhusu msiba huo, mjumbe wala mwenyekiti hawakufika pia. Jambo hilo lilimuumiza sana mzee Maboso akajiaminisha kuwa huwenda vifo hivyo ukawepo mkono wa mtu. Wakati mzee Maboso akiwaza suala hilo upande wa Zabro naye aliamini kama mzee Maboso alivyokuwa akiamini.
Baada ya msiba, mzee Maboso akamtaka Zabroni aishi nyumbani kwake, lilikuwa pigo baya sana katika maisha yake. Jambo hilo liliweza kumfanya asitishe zoezi la kuendelea kuiba, kwani aliyekuwa akimfanya aibe ameshapoteza maisha. Lakini licha ya kuamua kuacha zoezi hilo, ndani ya moyo wake kuna kitu alipania kukifanya mbadala. Roho ilimuuma sana, aliona hatolizika endapo kama kitu hicho hatokitekeleza "Nitahakikisha kila siku iendayo kwa Mungu nyumba moja inateketea kwa moto", alijisemea kwa uchungu ndani ya nafsi yake Zabroni, chozi halikusita kutiririka kunako mboni za macho yake. Akaona uamuzi wa kuchoma nyumba kila siku iendayo kwa Mungu ni uamuzi mzuri na sahihi pia. Uamuzi huo hakutaka kuufanya pasipo kumshirikisha mzee Maboso ambapo mzee huyo alimsifu sana Zabroni kwa kuamua kuchukuwa uamuzi wa kiume. Akaachia tabasamu bashasha kisha akasema "Safi Zabroni, upo sahihi. Samaki mmoja akioza, wote wameoza. Ukweli nina mashaka na uongozi wa juu kwenye hiki kijiji juu ya suala hili la kuwaawa kwa wazazi wako. Mimi nipo nyuma yako kijana wangu. Kesho nitakupa mzizi utautafuna, ni dawa ambayo itakufanya upotee katika mazingira yoyote pindi utakapo nuia maneno ambayo nitakwambia hapo kesho. Natamani lengo lako litatimia Zabroni ", tabasamu bashasha lilionekana usoni kwa Zabroni kupitia mwanga hafifu wa koroboi (Kibatali), baada tabasamu hilo akajibu." Nitakushuru sana, hakika nitachoma nyumba moja baada ya nyingine usiku usio julikana "
" Naam! Jasiri haogopi ", aliunga mkono mzee Maboso kisha akamtaka Zabroni atie unga unga kwenye maji waliyonjika jikoni, wasonge ugali wale ili kesho wagange yajayo.



Kesho asubuhi palipo pambazuka,mzee Maboso ndio alikuwa wa kwanza kuamka ambapo kabla ya yote alitoka nje kujisaidia kisha akarudi ndani. Alipo ingia ndani alimuamsha Zabroni na kumwambia "Mimi naenda kukagua mitego yangu nikirudi tupukuchue mahindi ili twende nashineni sionaona unga umetuishia?.." Zabroni aliposikia hiyo sauti ya mzee Maboso, haraka sana akakurupuka kutoka usinguzini na kisha akamjibu "Usijali hii kazi niachie mimi,we nenda kaangalie mitego yako babu wala usijali "http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sawa hamna shida ",alijibu mzee Maboso wakati huo akichukuwa panga na mkuki akaelekea porini kukagua mitego yake. Muda mchache Zabroni aliamka akanawa uso na kisha akaingia kwenye ghala kuchukuwa mahindi. Lakini kabla hajaanza kuyapukuchua,akaja Tina. Tina na Zabroni ni wapenzi, hivyo siku hiyo Tina alikuja kumuona Zabroni baada kuona muda mrefu hawajaonana na wala hana taarifa naye. Alifurahi sana kumuona mpenzi wake kwa mara nyingine, alizipiga hatua za kunyata ilihali Zabroni naye akionekana kuandaa mahali pakupukuchulia mahindi lakini alijikuta akizibwa macho na mtu ambaye hakumjua,ila baadaye kidogo Tina alitoa mikono yake kwenye macho ya Zabroni alicheka kidogo kisha akasema "Zasiku Tina"
"Safi Zabro,kwanza pole na matatizo. Lakini pia naomba unisamehe kwa kutokufika msibani. Wazazi walinikataza kufika mpenzi wangu", aliongea Tina kwa sauti ya chini huku akimtazama Zabroni kwa haibu Tina kwa sauti,Zabroni akamtoa shaka halafu akamjibu "Huna sababu ya kuniomba msamaha Tina,hayo ni mambo ya kawaida sana kwahiyo furahi kunikuta mzima". baada kusema hayo wawili hao waliketi chini wakaanza kupukuchua mahindi.
Wakati hayo yanajili, upande wa pili nyumbani kwa mwenyekiti alifika mzee Fungafunga. Fungafunga alionekana anamazungumzo na mwenyekiti siku hiyo ,kwa maana hiyo ilimbidi mwenyekiti aache kazi aliyokuwa akiifanya muda huo,alikuwa akitengeza mipini ya jembe. Sikio na mawazo yake akamkabidhi mzee Fungafunga ikamsikiliza mzee huyo ana jambo gani anataka kumwambia. Mzee Fungafunga akapewa kigoda akakaa,akakohoa kidogo kisha akaanza kusema "Naona kajua kanawaka"
"Mmh kiangazi hii bwana,kulikoni mbona leo hujaenda shamba"
"Nilikuwa namaongezi juu yako,ndio maana siku hii nimeamua iwe kwa ajili yako" alijibu mzee Fungafunga.
"Mmh sawa nakusikiliza"
"Kabla sijaingia kwenye jambo lanyewe hivi mipini huwa unatengeneza kwa shilingi ngapi?.."
"Aah bei poa tu kwa wewe elfu tatu tu"
"Anhaa. Sawa. Jambo lanyewe sasa ni kuhusu huyu kijana huyuuu.. Zabroni "
"Huyu mtoto wa marehemu mzee Ndalo? .."
"Huyo huyo,ujue tangu wazee wake wafariki tabia ya wizi imetoweka hapa kijijini"
"Kwa maana hiyo wanataka kusema yeye ndio alikuwa mwizi?". Fungafunga alikaa kimya kidogo kisha akajibu "Ndio maana yake! Au unaonaje?.." Mwenyekiti naye akakaa kimya muda mfupi halafu akajibu "Bila shaka naweza kuungana na wewe,sasa unanishauri nini?.."
"Mimi sina cha kukushauri ila nataka nikuulize swali! Vipi ukimfahamu muhusika wa tukio la kuchoma moto nyumba ya mzee Ndalo? .." mwenyekiti akashusha pumzi kwanza,akakohoa halafu akajibu "Kwa jinsi yule mzee nilivyokuwa simpendi,kiukweli nitampatia zawadi huyo muhusika. Unajua yule mzee tangu kipindi kile aninyime baiskeli yake nilimchukia sana na ndio maana hata msibani sikwenda,sio mimi hata balozi wangu nae hakwenda sijui wewe mwenzangu " Fungafunga aliposikia maneno hayo ya Mwenyekiti alicheka sana kisha akajibu "Wala sikwenda,kwanza mimi ndio muhusika wa tukio lile. Ukweli mzee Ndalo nilimuazima pesa kwa niaba ya matibabu ya mkewe lakini wakati wa malipo akaanza kunizungusha. Sikuwa na sababu nyingine mimi", Mwenyekiti alipigwa na butwaa kidogo ila mwishowe akarudi katika hali yake ambapo alikutana na Fungafunga akisema huku akianza kwa kucheka "Nipe zawadi yangu sasa"
"Baadaye tukutane kwa mama Ziada kuna ulanzi pale njoo tuburudike mzee mwenzangu kwani umekuwa shujaa ",alijibu Mwenyekiti, mzee Fungafunga akafurahi baada ya hayo akaaga na kuondoka zake nyuma akimuacha Mwenyekiti akilitafakari tukio lile huku akijiuliza kwanini baada wazazi wa Zabroni kuuwawa matukio wizi yametoweka kijiji hapo.
Kwingineko Zabroni na mpenzi wake ambaye ni Tina walikuwa wakiendelea kupukuchua mahindi,huku wakipiga zogo la hapa na pale. Baada kumaliza Tina aliaga kuwa anarudi nyumbani kwao,Zabroni aliamua kumsindikiza wakiwa njiani Zabroni akamwambia Tina "Tina najua ipo siku mimi nitafungwa jela,kwa sababu nitahitaji kulipa kisasi juu ya kifo cha wazazi wangu", Tina akastuka kusikia maneno hayo,akajibu "Unajua Zabroni mimi nimeshakuzoea,istoshe nakupenda sana. Je, unafikiri ukifungwa mimi nitakuwa katika hali gani? Hebu muachie Mungu ndio ataweza kukulipia"
"Tina dawa ya moto ni moto,acha nilipe kisasi? Lakini pia..." Kabla Zabroni hajaongea alichotaka kusema,mara ghafla mzee Fungafunga alifika. Tina ni mtoto wa mzee Fungafunga,ilihali mzee huyo ndio aliyehusika na mauaji ya wazazi wa Zabroni. Tina baada kumuona baba yake aliogopa sana,mara moja akatimua mbio wakati huo huo Zabroni naye aligeuka kurudi nyumbani ambapo alikutana uso kwa uso na mzee huyo. Mzee Fungafunga akamtazama Zabroni kwa jicho ngebe kisha akasema "Sitaki mazoea na mwanamgu mwana haramu wewe", Zabroni hakujibu neno lolote, alimtazama tu kisha akaishia zake. Lake rohoni.
Usiku ulipo fika,mzee Maboso alimkumbusha Zabroni kuhusu mzizi ambao utamfanya Zabroni kupotea popote pindi atakapo nuia na kisha kugusa kitu chochote.
"Hapa kila kitu kitakuwa sawa kijana wangu", aliongea mzee Maboso huku akiutoa mzizi huo kwenye kitambaa alichotumia kuhifadhia. Akaketi kwenye kigoda, akamtazama Zabroni kwenye mwanga hafifu wa kibatali, akaendelea kumueleza uwezo wa mzizi huo na maneno anayotakiwa kuyaongea pindi atakapo hitaji kupotea kwenye mazingira husika. "Kwahiyo unataka kuniambia kwamba nikishaongea maneno hayo halafu nikagusa kitu chochote iwe nyasi au ukuta napotea?..", aliuliza Zabroni kwa umakini zaidi.
"Naam! Hii dawa sio ya mchezo", alijibu mzee Maboso halafu akamkabidhi. Zabroni aliupokea mzizi huo, akautafuna. Alionekana kukunja uso wake, kwa namna gani mzizi huo ulivyokuwa mchungu. Baada kukamilika suala hilo, sasa akahitaji kufanya jaribio usiku huo huo. Alichomo moto nyumba nyumba tano, katika nyumba hizo hakubahatika kupona mtu hata mmoja. Kesho yake asubuhi, kijiji kikakubwa na janga kubwa la ajari ya moto, wanakijiji walimnyooshea kidole mwenyekiti wakati huo mwenyekiti akimtilia shaka mzee Fungafunga..
Mwenyekiti wa kijiji alimuhisi muhusika wa tukio hilo huwenda akawa ni mzee Fungafunga kwa maana jana alimwambia kuwa yeye ndio aliyehusika kuchoma nyumba ya mzee Ndalo,sasa hatimaye tukio hilo hilo limejitokeza tena. Istoshe limesababisha maafa mkubwa sababu ndani ya hizo nyumba tano zilizochomwa moto hakufanikiwa kutoka mtu hata mmoja,kitu ambacho kiliwasikitisha walio wengi ni familia ile iliyokuwa na watoto Saba pamoja na wazazi wao wawili. Familia yote ikawa imekufa kwa pamoja,huzuni kila pande ya kijiji wakati huo huo mzee Fungafunga akijiuliza "Nitaificha wapi sura yangu mimi mbele ya mwenyekiti? Sijui kwanini nilimwambia jambo lile",alijiuliza mzee Fungafunga huku akionekana kujilaumu jambo lile kumuelezea mwenyekiti ilimradi tu apate ujiko. Katika umati wa watu uliokusanyika katika nyumba ile ya familia saba,mwenyekiti akamtazama mzee Fungafunga kisha akamuita faragha. Mzee Fungafunga akionekana kuwa na hofu alitii wito wa Mwnyekiti.
"Mzee mwenzangu, nini sasa umefanya?" Mwnyekiti akamuuliza Fungafunga huku akionekana uso wake kana kwamba anataka kudondosha machozi,wakati huo huo mzee Fungafunga akashusha pumzi na kisha akajibu "Walaa sio mimi ndugu mwenyekiti, unafikiri kwa utu wangu huu naweza kufanya maafa kama haya? Hapana siwezi mwenyekiti labda tufanye uchunguzi atajulikana tu muhusika" alijibu mzee Fungafunga macho akiwa ameyatoa mfano wa chura aliyebanwa na mlango. Baada ya maelezo hayo mwenyekiti akajikuta akishindwa cha kuongeza kusema zaidi aliyafuta machozi yake yatokanayo na uchungu wa kupoteza baadhi ya wanakijiji wake, maana hali kijiji hapo ilionekana kutisha sana.
Wakati hayo yanaendelea, upande wa pili mzee Maboso na Zabroni walikuwa wakielekea shambani. Walipo kuwa njiani mzee Maboso akamwambia Zabroni "Nadhani umeona hiyo dawa ilivyokuwa noma"
"Dah! wewe acha tu,kwanza nilipofika kwenye nyumba ya kwanza nilichoma kumbe kwa mbali kuna mtu alikuwa anakuja maeneo hayo,bila shaka yule alikuwa mlevi maana usiku wote ule sio wa kutembea tembea hovyo. Basi bwana baada kumuona nikasema hapa haonwi mtu haraka sana nilinuia yale maneno halafu nikagusa ukuta wa nyumba hiyo hiyo nikawa nimepotea " Zabroni akacheka kwanza kisha akaendelea kusema "Nikasema kweli hii dawa ni moto wa kuetea mbali,na kwakuwa ni moto wa kuotea mbali? Hakuna budi kukamilisha methali ile isemayo dawa ya moto ni moto"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Naam upo sahihi Zabroni", aliunga mkono mzee Maboso na kisha wakagongena mikono wakacheka sana na zogo nyinginezo zikaendelea. Walifika shambani wakafanya shughuli zao mpaka mida ya saa nane mchana waliweza kurejea nyumbani kwao ambapo wakati walipofika tu nyumbani akaja mzee Adenel, mzee huyo alionekana anajambo moyoni mwake lakini pia mzee huyo hana uenyeji na kijiji hicho bila shaka alikuwa mgeni ingawa mzee Maboso alimfahamu fika na ndio maana alipomuona alionyesha kutabasamu.
"Karibu sana wanyumbani",alisema mzee Maboso huku akimlaki mgeni wake. "Nimeshakaribia,habari za siku nyingi ", alijibu mzee Adenel, mzee Maboso akaitikia "Salama sana ngoja nikachukue kigoda ili tukae tuongee zaidi ", baada kusema hayo mzee Maboso alizama ndani akachukuwa kigoda kisha akatoka nacho nje. "Enhe nipe habari hivi ni wewe kweli?..", alihoji mzee Maboso akionekana kutoyaamini macho yake lakini mzee Adenel akamjibu "Ndio ni mimi ujue miaka mingi sana nimekuacha hapa naona sasa tayari umekuwa mwenyeji wa Tanzania. Mmh sasa habari ni kwamba unatakiwa kurudi nyumbani. Familia inakuhitaji kwa vyovyote vile", aliongea mzee Adenel akimtaka Maboso arudi nyumbani kwao nchini Nigeria,mzee huyo alikuwa kiutafutaji kijijini hapo na hivyo mtafutaji ambaye alikuwa naye miaka ya nyuma kabla hajarudi nchini kwao leo hii kaja kumchukuwa. Hakika mzee Maboso alionekana kupoa huku sana mithiri ya maji ya mtungini, akawaza "Miaka mingi nipo nchi ya watu kiutafutaji sasa leo hii nirudi nyumbani sina kitu? Hakuna kilicho badirika Je, haibu yangu nitaificha wapi mimi?", aliwaza mzee Maboso kitendo kilicho pelekea ukimya kidogo kutawala lakini mwishowe kimya hicho kilitoweka baada mzee Adenel kumuuliza kwa lugha ya kikwao "Unawaza nini?"
"Hapana ila najiuliza nauli nitatoa wapi?.." alijibu mzee Maboso naye vile vile alijibu kwa lugha yao.
"Usijali kila kitu kipo cha muhimu wewe jiandae kesho turudi nyumbani"
"Sawa"
"Lakini mbona kuna mahala nimepita nimekuta watu wanaomboleza kulikoni kuna msiba?.." aliongeza Adenel. Mzee Maboso akamjibu "Ndio"
"Sasa kwanini hamjahudhulia",kabla mzee Maboso hajajibu,Zabroni alileta chakula maongezi hayo kuhusu misiba yakawa yamekomea hapo.
Usiku ulipoingia kesho yake ikiwa ndio safari ya mzee Maboso kurudi Nigeria, aliamwambia Zabroni kuhusu ujio na dhumuni la mzee Adenel. Zabroni aliumia sana kwani aliamini swahiba wake kuonana naye tena ni majaliwa hivyo alijiuliza amlipe nini? Ndipo akakumbuka kuwa alifukia fedha aridhini,fedha alizoiba zamani kwenye moja ya maduka kijijini hapo! Fedha hizo aliiba kwa kudhumuni ya kwenda kumtibia mama yake nje ya nchi, ndoto ambayo ilitoweka mithiri ya mshumaa uzimikapo unapokubwa na upepo. Haraka sana alikwenda kuzifukua kwa kuangalia ramani kilipokuwepo chumba chake, alifanikiwa kupaona. Aliachia tabasamu na kisha mara moja akaanza kuzifukua. Zoezi hilo lilikamlika, fedha zilikuwa kwenye mfuko wa gunia. Kwa mara nyingine tena akaachia tabasamu, akaona fedha hizo ni fadhila tosha kwa mzee Maboso aliyeamua kumuunga mkono juu ya hatua ya kulipa kisasi aliyochukuwa. Ni fedha nyingi mno.

Kesho palipokucha saa kumi na mbili safari ilianza,Zabroni akaambatana na wazee hao kuwasindikiza mpaka stendi ya magari yaendayo mjini,ikiwa kama hatua ya kwanza ya safari ya kuelekea Nageria Dakika tano nyingi gari ikawa imewadia maeneo hayo,mzee Maboso akamuaga Zabroni lakini kabla hajapanda gari, Zabroni alimpatia mfuko mdogo mweusi wenye fedha ambazo mzee Maboso hakuweza kutambua ni kiasi gani. Maboso akapanga gari na neno la mwisho alimwambia Zabroni "Mzee Fungafunga ndio muuwaji wa wazazi wako,nakutakia kazi njema kijana wangu ",kwisha kusema hivyo gari iliondoka pole pole mpaka kasi ilipoongezeka. Huku nyuma kijana Zabroni akionekana kupigwa na butwaa akajiuliza "Yani inamaana kwamba baba yangu mkwe mtarajiwa ndio kafanya kitendo hiki Mzee Maboso hajawahi kunidanganya, acha nitembeze moto sasa mpaka kijiji kiwe jangwa. Tina utanisamehe maana hili ni pigo lisilo saharika katika maisha yangu" kwisha kuwaza hayo Zabroni akidondosha machozi ya hasira.


ITAENDELEA


(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

No comments:

Theme images by imagedepotpro. Powered by Blogger.