Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi sehemu ya saba (7)

Kulipokucha, Sabrina ndiye
alikuwa wa kwanza kuamka na alichofanya ni kwenda kukichukua kile kiboko ili
kukirudisha kwa Sakina kabla ya mama yake kukiona.
Alipofika kwa Sakina alimkuta nae ndio ametoka kuamka na kuanza kumueleza
yaliyojiri usiku
"Ile dawa kweli ni khatari dada maana hadi nimejishangaa kupata ule
ujasiri jamani"
"Ile dawa ilikuwa inakuwa wewe ujasiri halafu inamzubaisha yule mchawi.
Ila usingemsemesha, ningekuja kumuona na mimi"
"Kumbe nisingemsemesha asingeondoka eeeh!"
"Ndio, ila ulipomsemesha ndio ukamzindua na kumfanya aweze kuondoka. Na je
umemchapa viboko vingapi?"
"Vitatu kama ulivyosema"
"Vizuri sana Sabrina"
Hakutaka kusema ukweli kama kamchapa viboko vinne ili Sakina asichukie kwavile
amekiuka masharti waliyokubaliana nae.
Baada ya hapo alirudi kwao ili kujiandaa kwaajili ya safari aliyopanga na
Francis.
Alitafuta ile nguo yake nzuri kabisa tena ya heshima ili akionekana aweze
kukubalika ukweni bila ya tatizo lolote.
Hadi muda anapigiwa simu alikuwa tayari ameshajiandaa vya kutosha na kwenda
kuonana na Francis.
Kwanza kabisa akaenda nae kwa Sakina ili aweze kuwasaminisha
"Mmh Sabrina mdogo wangu umependeza sana"
"Asante dada"
"Na wewe Francis angalia bhana, tena tafadhari sana usimuumize mdogo
wangu. Nampenda sana huyu"
"Usijali dada, nakuahidi sitokuja kumuumiza kamwe katika maisha yake.
Nampenda sana na ndiomana leo nimejitoa ili nimpeleke kwa ndugu zangu
wamjue"
Sabrina alikuwa akifurahi tu muda wote kwani aliona fahari kila aliposikia neno
nakupenda toka kwa Francis.
Sakina aliwapa baraka zake kisha nao wakaendelea na safari zao.
Njiani, walikutana na yule mwanamke ambaye Sabrina aliwahi kumfanyia fujo.
Walipopishana nae, yule mwanamke alimsonya Sabrina kisha akamwambia
"Dawa yak o inachemka wewe"
Na kuwapita pale, Francis alimuangalia Sabrina na kumuuliza
"Kwani vipi na huyo mwanamke?"
"Ni mchawi huyo"
"Unawezaje kuwekeana visasi na wachawi Sabrina?"
"Ni historia ndefu sana ila tuachane nayo kwanza"
Wakaendelea na safari yao.
Walipofika kwa bibi yake na Francis waliwakuta watu wakiwa kimya sana, kisha
wakakaribishwa vizuri sana na kumfanya Sabrina azidi kupata furaha ya moyo.
Kisha Francis akamuuliza nduguye mmoja alipo bibi yake ili aweze kumtambulisha
Sabrina
"Eti bibi yuko wapi?"
Akijibu huku amenyong'onyea,
"Bibi anaumwa"
"Anaumwa? Tangu lini? Na mbona hamkuniambia?"
"Ni leo tu ndio ameamka vibaya, tena tulitaka tukupigie simu. Afadhari
umekuja mwenyewe"
"Kwahiyo yuko wapi?"
"Kalala tu chumbani kwake, hajiwezi kwakweli"
Francis akainuka na kwenda kumuangalia bibi yake kipenzi, akamuhurumia sana
kwani bibi yake hakuweza hata kuzungumza.
"Pole sana bibi yangu"
Aliongea huku machozi yakimlengalenga kwani alimpenda sana, bibi nae aliitikia
kwa kichwa tu pale pale kitandani.
Kisha Francis akamuomba bibi yake kuwa amletee mchumba wake japo amuone tu,
bibi akaitikia kwa kichwa kisha Francis akaenda kumchukua Sabrina.
Akaenda nae chumbani kwa bibi yake, Sabrina kufika pale macho yake yakagongana
na macho ya yule bibi na kufanya ashtuke kwani alikuwa ni yule yule mmama
aliyempiga usiku.
Akaenda nae chumbani kwa bibi yake, Sabrina kufika
pale macho yake yakagongana na macho ya yule bibi
na kufanya ashtuke kwani alikuwa ni yule yule
mmama aliyempiga usiku.
Sabrina akaogopa sana na hakuweza kuzuia uoga wake kwani yule bibi alimkazia
sana macho na kumfanya atetemeke na kutoka nje huku anakimbia.
Francis akamfata nyuma na kumuuliza,
"Kwani nini Sabrina?"
Kama kawaida yake ya kuropoka akajikuta akimwambia Francis
"Yule bibi ni mchawi"
Bila kujua kama kauli hiyo ingewezaje kumbadilisha Francis
"Unasemaje Sabrina?"
Sabrina akaongea kwa kujiumauma sasa na kujilaumu kuwa kwanini ameropoka vile
"Samahani Francis"
"Yani unamuita bibi yangu mchawi halafu unaniomba samahani kirahisi
tu!"
"Naomba unisamehe Francis"
Francis alikuwa amechukia sana kwa kile kitendo cha bibi yake mpenzi kuitwa
mchawi
"Yani siamini kabisa kama wewe Sabrina unaweza kumuita bibi yangu mchawi,
siamini kwakweli"
"Nisamehe jamani"
"Usitake nitende dhambi Sabrina, tafadhari naomba uende. Kwa usalama wako
nenda"
Kwa jinsi Francis alivyokuwa akiongea kwa ukali ilimbidi Sabrina aondoke huku
moyo ukimuuma sana na kujilaumu kwa kuropoka kwake ingawa ilikuwa ni kweli ila
ndio ilishamponza tayari.
Wakati Sabrina anatoka kwenye ile nyumba, akakutana na kijana aliyekuwa anataka
kuingia mule ila alipomuona Sabrina akitoka huku machozi yakimbubujika
alimuonea huruma na kumfata.
"Nini tatizo dada?"
"Hamna kitu"
"Mbona unalia sasa?"
Sabrina alizidi kutokwa na machozi tu, yule kijana akamshika Sabrina mkono na
kumrudisha ndani ya geti la ile nyumba ili amuhoji vizuri kinachomliza.
Alipomrudisha tu, Francis nae alitoka nje na kuchukizwa kwa kuendelea kumuona
Sabrina eneo lile, kisha akamwambia nduguye aliyemshika Sabrina mkono
"Fredy, mwache huyo malaya aende zake"
"Kwani amefanyaje?"
"Achana nae bhana"
Kile kitendo cha Sabrina kusikia kuwa yeye akiitwa malaya kilimuuma sana tena
zaidi hata alivyoumia mwanzo kwani hakuamini kama Francis huyu aliyemwambia
kuwa anampenda kwa vyovyote vile leo hii anamfukuza na kumuita malaya kisa tu
kaongea ukweli, roho ilimuuma sana na kuondoka huku akilia zaidi ila Francis
hakujali chochote.
Fredy, alimfata Francis ili kumuuliza vizuri
"Kwani kafanyeje yule?"
"Mwanamke fala sana yule, ndio kwanza leo namleta halafu anamuita bibi
yangu mchawi! Na akafie mbele huko"
"Kwahiyo ni sababu hiyo tu iliyokufanya umfukuze?"
"Tena sio kumfukuza tu, yani hata kumuona sitaki yani sitaki kabisa"
"Mmh ulimpenda kweli yule mwanamke wewe?"
"Nilimpenda ndio ila siwezi kuvumilia upuuzi kama huu kwakweli"
Francis alionekana kuwa na hasira sana kupita maelezo ya kawaida na kuingia
tena ndani.
Moyo wa Fredy bado ukamtuma kuwa amfate yule binti, kisha akatoka na kuanza
kumfatilia.
Kwavile Sabrina alijihisi kuchanganyikiwa hadi akasahau njia waliyokuja nayo
mwanzo na kujikuta akipita njia nyingine.
Isingekuwa Fredy kumfata basi angepotea leo.
Fredy alimuuliza,
"Kwani unaenda wapi?"
"Nataka kwenda kupanda daladala nirudi nyumbani"
"Dah huko uendako unapotea dada, twende nikupeleke stendi"
Kisha Sabrina akaanza kufatana pamoja na Fredy ambaye alipanda nae daladala
hadi akamfikisha kwao kabisa.
"Asante sana"
"Usijali, mimi ni kati ya wanaume walioumbwa na moyo wa huruma katika
dunia hii. Nimekuhurumia sana ndiomana nikafanya haya"
"Nashukuru sana kaka"
"Naitwa Fredy, vipi wewe jina lako!"
"Naitwa Sabrina"
"Sawa Sabrina tutawasiliana basi"
Kisha Fredy akampa namba zake Sabrina na kumuaga pale halafu akaondoka.
Sabrina aliingia ndani kwao ila mama yake hakuwepo na kumfanya apate muda
muafaka wa kuwaza yanayomsibu.
"Mmh sijui nikamuhadithie dada Sakina! Lakini ataniona ni mpumbavu. Ngoja
nijaribu kukaa nalo moyoni huku nikiombea Francis anisamehe jamani"
Alikuwa akiwaza sana huku akiumia moyoni mwake.
Baada ya masaa kupita akajaribu kumpigia simu Francis lakini simu yake
haikupokelewa na kumfanya aumie zaidi na zaidi.
Muda kidogo alifika mgeni nyumbani kwao na mgeni huyo alikuwa ni Sakina
"Kheee Sabrina, umerudi saa ngapi?"
"Muda tu, karibu"
"Mi nimemfata mama yako"
"Na hata hayupo"
Ila Sakina alimgundua Sabrina kuwa hayupo sawa ingawa kila alipomdadisi kuhusu
alipotoka hakusema ukweli na kuishia kujibu kuwa ni nzuri tu.
"Niambie ukweli Sabrina, najua una matatizo niambie tafadhari"
Baada ya kumbana sana, Sabrina akaamua kusema ukweli kwa Sakina kwa yale yaliyojiri
"Mungu wangu Sabrina, kheee kwani wewe ulimchapa viboko vingapi jana"
Napo ilibidi aseme ukweli kuwa alimchapa viboko vinne tofauti na alivyoambiwa
"Hayo majanga mdogo wangu, kwanini ulifanya tofauti na nilivyokwambia?
Haya swali jingine sasa, kama huyo bibi ni bibi yake huyo Francis kwanini
alikufata wewe kukuwangia?"
"Hata mi mwenyewe sielewi dada yani sielewi kabisa na hata sijui cha
kufanya maana Francis nampenda ila sijui itakuwaje. Sijui kama ataendelea na
mimi kwa jinsi alivyonifukuza"
Sakina alimuhurumia sana Sabrina na kumpa moyo
"Usijali, atakusamehe tu wala usiwe na wasiwasi"
Muda mwingi Sabrina alijilaumu mdomo wake kwa kuropoka mambo yasiyotakiwa
kuropokwa kama hili linalompa mawazo kwasasa na kumkosesha raha ya maisha na
kumfanya akose furaha.
Usiku ulipofika alimkumbuka sana Francis lakini kila alipojaribu kumpigia simu,
simu yake haikupokelewa. Hata alipojaribu kumtumia ujumbe, jumbe zake
hazikujibiwa na kumfanya azidi kupatwa na mawazo yasiyo rasmi.
Akaamua kuitafuta ile namba aliyopewa na Fredy ili amuulizie Francis kwa Fredy
"Unaongea na Sabrina hapa"
"Ooh! Kumbe Sabrina, nipe khabari"
"Namuulizia Francis, anaendeleaje?"
"Yuko poa, ila acha kujiumiza kichwa kwa hayo mambo wangu. Utaumia bure,
kesho kama unamuda basi tuonane. Sawa?"
"Hakuna tatizo basi"
Akamuaga na kukata simu huku akiamini kuwa huyu Fredy ndiye atakayemsaidia yeye
kuwa na mahusiano tena na Francis.
Kesho yake alimuaga mama yake na kwenda kuonana na Fredy kama ambavyo walipanga
kwenye simu.
"Kwani Francis mlifahamiana vipi?"
Sabrina alimueleza Fredy kwa kifupi tu.
"Nimekuelewa, sasa una mpango upi baada ya yote"
"Nampenda Francis, nahitaji anisamehe ili niwe nae tena"
"Poa usijali, ila kama akikataa kukusamehe usiwe na shaka. Wengine tupo
hapa"
Aliongea kwa utani lakini ndio alikuwa akimaanisha hivyo kwani nae alijikuta
akimpenda Sabrina na kuvutiwa nae.
Waliongea mambo mengi sana, kisha wakaagana na kuondoka.
Sabrina alirudi kwao huku akiwa na imani kwamba atasaidiwa na Fredy kuweza
kurudiana na Francis bila kujua kwamba Fredy nae kashampenda tayari na hatoweza
kufanya kitu hiko cha kumsaidia.
Maisha yao nayo yakaendelea kwa mtindo huo huku Fredy akidumisha mawasiliano na
Sabrina.
Toka lile sakata la Sabrina kumpiga yule mchawi usiku, hakuweza tena kufatwa na
hao wachawi kwa kipindi hiko na bado hakujua kwanini bibi yake Francis
alimfata.
Alitamani sana kujua ni kwanini ila hakuweza kujua kabisa.
Mawasiliano baina yake na Fredy yalishamiri sana.
"Naomba kesho nikutembelee kwenu hapo Sabrina"
"Karibu tu hata usijali, wee njoo tu"
Fredy alifurahi kwani alijua ndio sehemu ya kwenda kubwaga ya moyo wake.
Kesho yake Fredy alienda kwa wakina Sabrina na kumkuta, ile leo hakumkuta mama
yake na Sabrina kwavile alitoka.
"Eeh niambie Francis anaendeleaje, maana hapokei simu zangu wala hajibu
meseji zangu"
"Francis kanipa ujumbe kuwa usimsumbue tena, na hivi ninavyokwambia ana
mwanamke mwingine. Kwakweli nimekuhurumia sana Sabrina kwa kung'ang'ania sehemu
usiyotakiwa wakati wapo watu wa maana tu wanaokuhitaji kushinda hata huyo Francis"
"Wakina nani hao?"
"Mimi hapa, kwakweli nakupenda sana Sabrina. Siku zote hizi nimekuwa
nikikupenda sema tu sikujua nianzie wapi kukwambia"
"Mmmh Fredy!"
"Sikutanii Sabrina, mi ni msema kweli na huo ndio ukweli kutoka moyoni
mwangu"
"Wewe si ndugu yake na Francis! Halafu si unamwanamke wewe!"
"Sina mwanamke mie, nakupenda wewe Sabrina. Ni kweli Francis ni ndugu
yangu ila yeye alikutamani, mimi ndiye ninayekupenda. Mungu alifanya makusudi
kukukutanisha wewe na Francis ili uweze kukutana na mimi mwenye mapenzi ya
dhati na wewe. Sina nia mbaya naye zaidi ya upendo wa dhati"
Maneno ambayo Fredy alikuwa akiyaongea yalimuingia akilini Sabrina na kujikuta
akivutiwa nae huku akiwaza kuwa anayoyasema yanaweza kuwa yana ukweli ndani
yake.
"Basi tutaongea vizuri kwenye simu badae"
Hakutaka kumjibu kwa muda huo kwavile bado alimpenda Francis ingawa maneno ya
Fredy nayo yalimuingia kichwani.
Wakaongea mengi kisha Fredy akaaga na kuondoka halafu Sabrina akamsindikiza.
Wakati Sabrina anarudi kutoka kituoni alipotoka kumsindikiza Fredy.
Njiani alijikwaa kwenye jiwe na kuanguka, alipojitahidi kuinuka aliona damu
zikimtoka kwenye kidole, alikuwa amechunika ngozi kwenye dole gumba la mguu wa
kushoto na damu kiasi zilimwagika pale.
Alijikongoja hadi nyumbani kwa Sakina kwavile hapakuwa mbali sana na
alipojikwaa.
Sakina alipomuona alimshangaa
"Vipi mbona unachechemea Sabrina?"
Sabrina akamuonyesha kile kidole na kumueleza alivyojikwaa.
Sakina akachukua pamba na kumfuta Sabrina kisha akamfunga pale kwenye kidole.
Wakati anamalizia kumfunga ikawa kama mtu aliyekumbuka kitu na kumuuliza
"Umejikwaa sehemu gani?"
"Pale karibia na kiwanja, pale kwenye njiapanda"
"Mmmh!!"
"Mbona unaguna?"
Akamfunga haraka haraka na kumwambia
"Hebu twende ukanionyeshe"
Wakainuka na kwenda mahali alipojikwaa Sabrina.
Kufika pale, walikuta ile sehemu ambayo damu ya kwenye kidole cha Sabrina
imemwagika ikawa kama mtu kaja kuichota na mchanga wake na kuacha kijishimo.
"Umeona Sabrina?"
"Nimeona"
"Inamaana hapa kuna mtu kaichota damu yako"
"Sasa kwanini kaichota?"
"Unafatiliwa Sabrina, yani ni bora tungekumbuka muda ule ule ila bado
hatujachelewa sana. Nisubiri kidogo tena hapa hapa usiondoke"
Sakina akaondoka na kumuacha Sabrina mahali pale.
Baada ya muda kidogo akarejea na kimfuko kidogo, ndani yake alibeba majivu na
kipande cha mkaa, kisha akamwambia Sabrina
"Kwavile yeye alisahau kufukia hiki kishimo wakati anachukua damu yako
basi tutakifukia sie"
Akachukua kale kamkaa kadogo na kuweka kwenye kale kashimo halafu akaweka
majivu juu yake kisha akasawazisha na mchanga pale juu na kumwambia Sabrina
kuwa waondoke.
Waliporudi nyumbani, Sakina akamuonya tena Sabrina
"Usimwambie mama yako"
"Ila dada leo hebu niambie kwanini hutaki nimwambie mama?"
"Mama yako yule ni mtu wa maombi kwahiyo ataharibu kila kitu ndiomana
sipendi umwambie"
"Hapo nimekuelewa sasa"
Kisha akarudi nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa ndani.
"Haya niambie, pale njiani mlikuwa mnafanya nini na Sakina wako?"
Sabrina akashtuka kugundua kwamba mama yake aliwaona, ikabidi amdanganye
"Tulikuwa tunaongea tu mama, kuna mgeni tulimsindikiza"
"Endelea kunificha mwanangu ila ipo siku kila kitu kitakuwa peupe"
Joy alihisi tu kuwa kuna vitu mtoto wake anamficha ila hakutaka kumlazimisha
sana kuwa amwambie kwani alijua ipo siku lazima atasema yeye mwenyewe bila hata
ya kushurutishwa.
Siku hiyo ikapita, hata usiku wake ukapita vizuri kabisa bila ya tatizo lolote.
Kitu kimoja tu kilichomtatiza Sabrina ni kamba yake ya kiunoni na ilikuwa ni
siri yake yeye na Sakina, hakutaka mtu mwingine ajue hiyo siri haswaa Fredy.
Wakati akiwaza kuhusu huyo Fredy na kukiambia kichwa chake kiamue moja kama
kumsubiri Francis arudishe moyo au kuwa na Fredy.
Muda huo huo akapigiwa simu na huyo Fredy
"Naomba tuonane Sabrina"
Sabrina hakukataa na wakapanga mahali pa kwenda kukutana, ambapo waliona kuwa
sehemu nzuri ni ufukweni ili waweze kufikia muafaka wa swala lao.
Muda wa kuonana ulifika, wote wawili waliwahi kufika eneo la tukio.
Walikaa kwenye mchanga na kupeana habari mbalimbali.
Wakati wakizungumza, Fredy alijikuta akipatwa na matamanio zaidi juu ya Sabrina
na kumfanya awe nae karibu zaidi hata aweze kumshikashika ili aridhike.
Wakati yupo karibu vile, akazungusha mkono wake kwenye kiuno cha Sabrina na
kujikuta akiishika ile kamba.
Bila uvumilivu akamuuliza Sabrina
"Unavaaga shanga?"
Sabrina nae akashtuka na kujibu
"Hapana, sivaagi"
"Sasa hii naishika kwenye kiuno chako ni nini"
Sabrina akaogopa kujibu na kuutoa mkono wa Fredy kwenye kiuno chake.
"Niambie Sabrina, kitu gani hicho?"
"Sio kitu"
Fredy alitamani sana kujua kuwa ni kitu gani, wakati wanaendelea na maongezi,
Fredy akamfunua Sabrina blauzi kwa kumshtukiza ili aone kile cha kiunoni.
Muda anakitazama tu ni muda huohuo Sabrina akashtuka na ni muda huohuo Fredy
nae akaanguka chini kwenye mchanga huku damu zikimtoka machoni.
Fredy alitamani sana kujua kuwa ni kitu gani, wakati
wanaendelea na maongezi, Fredy akamfunua Sabrina
blauzi kwa kumshtukiza ili aone kile cha kiunoni.
Muda anakitazama tu ni muda huohuo Sabrina
akashtuka na ni muda huohuo Fredy nae akaanguka
chini kwenye mchanga huku damu zikimtoka
machoni.
Hofu ikampata Sabrina, alihisi kuchanganyikiwa kwa muda huo na hakujua ni kitu
gani afanye ili kukabiliana na ile hali.
Aliangalia watu pale ufukweni kama kuna yeyote anayewatizama ila kila mmoja
alikuwa akiendelea na mambo yake kanakwamba hawaoni kinachoendelea.
Sabrina alitamani hata akimbie na kumuacha Fredy pale ila moyo wake ulimsuta.
Akapata wazo la kumpigia simu Sakina, na hakutaka kupoteza muda kisha akachukua
simu na kumpigia.
Wakati Sakina anapokea ile simu tena kabla hata ya Sabrina kuongea nae kitu
chochote kile alishangaa kumuona Fredy akiinuka pale chini tena akiwa hana hata
tone la damu kwenye macho wakati mwanzoni macho yake yalikuwa yakitoa damu.
Sabrina akashtuka sana na kushindwa kuongea chochote na Sakina hata Sakina
mwenyewe alishangaa kwani alikazana kusema "Hallow, hallow" bila ya
majibu ya aina yoyote ile hadi akaamua kuikata ile simu tu.
Sabrina alikuwa kama mtu aliyepigwa na butwaa, hakuelewa chochote kwa wakati
ule.
Fredy nae alipoinuka pale akaanza kulalamika kuwa kichwa kinamuuma hivyobasi
akamuomba Sabrina waondoke. Sabrina hakukataa kwani naye alishachanganyikiwa
tayari na akaona kuwa labda waondoke mahali hapo na kurudi makwao tu.
Sabrina alirudi nyumbani kwao huku akiona akili yake kuwa imepagawa.
Moja kwa moja alienda kulala kwani alijihisi kuumwa kichwa pia kwa kutafakari
kitu asichokielewa.
Usiku kwenye mida ya saa mbili alimsikia mama yake akimuita, alipotoka nje
alishangaa kumuona baba yake.
Alifurahi sana ingawa baba yake alirudi bila ya kuwapa taarifa.
"Jamani baba, hata bila ya kusema!!"
"Nilitaka kuwafanyia surprise kama hivi mwanangu"
Wote walikuwa na furaha kwa ujio wa baba wa mwenye nyumba.
Hata Sabrina aliporudi kulala akawa amesahau yote yaliyomtokea kutokana na
furaha aliyokuwa nayo kwa wakati huo wa usiku.
Kesho yake, asubuhi na mapema, Sabrina alipigiwa simu na Fredy
"Sabrina, kwanini umenifanyia hivi?"
"Nimekufanyia nini Fredy?"
"Inamaana hujui ulichokifanya!"
"Niambie Fredy, sijui chochote"
Fredy akakata ile simu na kumfanya Sabrina apatwe na mawazo kwavile hakujua
kuwa ni kitu gani kimemtokea Fredy mpaka akasema vile tena asubuhi kabla bila
hata ya salamu.
Sabrina akapata wazo la kwenda kwa Sakina ili amwambie yaliyojiri na pia aweze
kupata ushauri kutoka kwake.
Alifika kwa Sakina na kumkuta kama kawaida yake, naye akamkaribisha vizuri sana
na kama kawaida ya Sabrina hakutaka kupoteza wakati hivyobasi akamsimulia
Sakina mambo yote yaliyojiri juu yake.
"Kheee mbona makubwa hivyo Sabrina!!"
"Ndio hivyo dada, yani hapa hata sijui cha kufanya dada yangu"
"Hayo mambo ni makubwa sana Sabrina, itabidi nimtafute mtu akakuulizie
kuwa ni kitu gani"
"Itakuwa vizuri sana dada"
"Haya niambie, na huyo mwanaume kwani umemfanya nini hadi
akakulalamikia?"
"Hata sielewi dada yangu, mi mwenyewe nimeshangaa tu akinilalamikia. Sijui
ni kitu gani, itabidi nimuulize vizuri"
Sabrina akaongea mambo mengi sana na kushauriana vitu vingi sana huku wakipanga
namna ya kukabiliana na matatizo yanayomzunguka Sabrina.
Baada ya kuridhika na mazungumzo yale, Sabrina aliamua kurudi kwao sasa.
Alipofika kwao, moja kwa moja akamkuta mama yake na baba yake wakiongea.
Ile alipotokea tu, mama yake akasema
"Umemuona mtoto wako! Basi ndio tabia yake siku hizi, pakikucha tu mwanao
anaona miguu inamuwasha. Basi yuleee kiguu na njia kwa majirani"
"Anaendaga wapi kwani?"
"Wapi kwingine zaidi ya kwa Sakina! Yani huyo Sakina ndio amekuwa mama
yake na baba yake hapo unapomuona, kila kitu anamueleza Sakina tu"
Bwana Deo akasikitika sana na kumuita Sabrina ili ajaribu kumuuliza vizuri, ila
kama kawaida ya Sabrina maelezo yake yalipindapinda na kumfanya baba yake apate
wazo la kufanya dhidi yake.
"Nenda tu, najua cha kufanya"
Sabrina akainuka na kwenda kuendelea na mambo yake mengine bila ya kujua kuwa
baba yake ameamua kufanya kitu gani dhidi yake.
Usiku ulipofika aliamua kuwasiliana na Fredy ili kujua kuwa ni kitu gani
alichomfanyia
"Ni kweli unataka kujua?"
"Ndio, nahitaji kujua Fredy"
"Kujua unajua ila tu unajipumbaza, ila kama unahitaji kujua kwa undani
zaidi nakuomba kesho tuonane"
"Hilo halina tatizo Fredy, tutaonana tu"
Fredy akakubaliana na Sabrina mahali pa kukutaniana siku ya kesho ingawa
hakumtajia kuwa wataenda kufanya kitu gani, na kumfanya Sabrina kuwa mgumu sana
kuelewa juu ya hilo.
Sabrina alipokuwa amelala usiku, ikamjia njozi.
Alihisi kuna watu watatu wameingia kwenye chumba chake tena kwa staili zilezile
ambazo wachawi huwa wanaingia, wale watu wakamnyanyua Sabrina pale kitandani
kwa madawa yao kisha Sabrina akaanza kuwafata kama wanavyomuelekeza.
Yani ilikuwa kama roboti zinavyopelekwa na mashine ndivyo ilivyokuwa kwa
Sabrina, akafikishwa mahali halafu akafanywa kama meza.
Wale watu walikuwa wakicheza na kula nyama, mara nyingine walimkalia kwa juu
kama kiti, mara nyingine walimuwekea chakula juu yake kama meza na mara
nyingine walimfanya kama punda au farasi, kwamaana kwamba walipanda juu yake
kisha Sabrina akawa anawatembeza kama ambavyo farasi hufanya.
Mambo mengi yalifanyika ila kwa Sabrina ilikuwa kama njozi tu.
Muda ulifika wakaanza kumpa maelekezo mengine kama ya kumrudisha kwao,
wakampeleka tena hadi chumbani kwake kitandani ila wakasahau kumuosha miguu.
Ila walipotaka kumchukua tena ili wakamnawishe, ndio hapo hapo Sabrina
akashtuka kutoka kwenye ile njozi na ilikuwa ni alfajiri tayari.
Sabrina aliinuka kutoka usingizini na kukaa huku akiwaza ile ndoto kuwa ni ya
aina gani! Ila alijihisi kuchoka sana kwa viungo vyake, haswaa mgongo ambao
ulikuwa ukimuuma sana kwa wakati huo.
Akajaribu kujinyoosha lakini bado maumivu aliyasikia mwilini na kumfanya
atafakari vizuri zaidi kuwa ile ni ndoto au ni kweli.
"Mbona sijielewi sasa! Hivi nilikuwa naota au ni kweli ilikuwa vile
usiku!!"
Hakupata jibu, ila alipojitazama miguuni alishtuka zaidi baada ya kuona miguu
yake imejaa vumbi
"Mungu wangu, inamaana ni kweli? Inamaana wachawi walikuja kunibeba
usiku!"
Hofu ikamjaa na kumfanya palipokucha vizuri tu aende kwa Sakina kumuelezea yale
mambo.
Alipofika kwa Sakina hakumkuta na kumfanya ajiulize kuwa asubuhi ile amekwenda
wapi, na alipojaribu kupiga simu yake haikupatikana. Ilikuwa ni ajabu sana kwa
Sabrina na kumfanya apatwe na mawazo zaidi na kuamua kurudi kwao tu.
Alimkuta baba yake akiwa amekaa sebleni na kumsalimia
"Kumbe ni kweli mwanangu kuwa ikifika asubuhi miguu inakuwasha!"
"Hapana baba, nilikuwa hapo nje tu"
"Hapo nje kwetu ndio siku hizi kuna vumbi kiasi hicho mwanangu!!"
Sabrina akajitazama tena miguuni, akatamani kumwambia baba yake ukweli kuhusu
mambo yaliyojiri na ndoto aliyoota usiku lakini midomo yake ilikuwa mizito
kusema na kujikuta akimuangalia tu baba yake bila ya kumwambia kitu cha aina
yoyote ile.
Deo alimtazama sana binti yake na kujaribu kuitafakari akili ya mwanae bila ya
majibu yoyote yale, kisha akamruhusu kuwa aende akaendelee na shughuli
nyingine.
Sabrina alienda kuoga moja kwa moja.
Alipokuwa anaoga alijishika kiunoni na kuona hali sio ya kawaida kwani ile
kamba haikuwepo tena kwenye kiuno chake.
Sabrina alijaribu kutafakari bila majibu,
"Imeenda wapi ile kamba? Mbona maajabu haya! Au yule bibi alinihurumia
akaitoa?"
Sabrina hakupata jibu zaidi ya kujiongezea maswali na mawazo katika kichwa
chake.
"Sijielewi kwakweli, kitu gani kimetokea kwangu? Na kimetokeaje? Na
kwanini kimetokea? Mbona sipati jibu?"
Hakuwa na raha kabisa, hata alipomaliza kuoga bado alikuwa na mawazo na kumfanya
ashindwe kufanya kitu cha aina yoyote ile.
Mchana akapigiwa simu na Fredy
"Sabrina, kama tulivyoongea usiku. Tukutane pale Mitini guest house"
"Sawa hakuna tatizo ila hujaniambia kuwa tunaenda kufanya nini hapo"
"Nimekwambia utajua huko huko"
"Poa, hakuna tatizo"
Fredy akashangaa kwa Sabrina kuitikia haraka hivyo wakati usiku wa jana yake tu
alikuwa akipinga swala hilo ingawa badae alikubali kwa kusitasita ila leo
alikubali moja kwa moja bila mashaka ya aina yoyote ile.
Mawazo ya Sabrina yalimpelekea kwamba Fredy anahitaji kulala nae na ndiomana
kamwambia wakutane huko kwenye nyumba za kulala wageni.
"Mmh nitaweza kweli kulala na mwanaume? Sijui itakuwaje, nitajua hukohuko
ila bora kamba imetoka"
Sabrina hakuwahi kukutana kimwili na mwanaume yeyote yule na ile kamba ndiyo
iliyokuwa ikimpa mashaka zaidi kuwa hakuna mwanaume atakayeweza kumuelewa
ukizingatia kamba yenyewe ilikuwa na muonekano wa hirizi.
Kwavile sasa ile kamba haikuwepo tena kiunoni mwake, akaona sasa ni wakati
muafaka kwake kwenda kujaribu ukizingatia Fredy mwenyewe ndiye aliyetaka na
kumuita.
Mida ilipofika, Sabrina alijiandaa na kwenda kumuaga mama yake
"Haya wapi sasa?"
"Naenda kwa rafiki yangu mama"
"Sabrina, Sabrina. Kuwa makini mwanangu na hizo safari zako
zisizoeleweka"
"Usijali mama, niko makini"
Kisha akamuaga na kuondoka.
Safari ilikuwa ni moja kwa moja alikopanga kukutana na Fredy.
Njiani akakutana na mmama mmoja, yule mmama alipita karibu na Sabrina kisha
akacheka.
Sabrina akamuangalia yule mmama na kumshangaa kuwa kilichomchekesha ni kitu
gani, kisha yule mmama akamwambia Sabrina
"Na bado"
Halafu akaondoka, Sabrina alikuwa na mshangao tu pale aliposimama kwani
hakumuelewa kabisa yule mmama.
Wakati anaendelea na safari, wazo likamjia. Taswira ya yule mmama ikamji kuwa
ni kati ya wale watatu aliowaona ndotoni ambapo bado anamashaka kuwa ni ndoto
au ni ukweli. Ila kwa ile hali ilivyoonekana akapata jibu kuwa ile haikuwa
ndoto tu bali ni ukweli mtupu.
Akaamua kuendelea na safari yake ingawa mawazo yaliendelea kuitafuna akili yake.
Alifika mahali walikopanga kukutana na Fredy, kisha Sabrina akampigia simu
Fredy ili ajue alipo
"Nishafika Fredy uko wapi?"
"Ingia moja kwa moja ndani, chumba namba tano"
Sabrina hakujishauri sana, alipokata simu tu akaelekea ndani hadi kwenye chumba
alichoelekezwa na Fredy.
Alipofika alifungua mlango na kumkuta Fredy amejilaza kitandani.
Moja kwa moja Sabrina alimuuliza Fredy,
"Mbona umejilaza hivyo?"
"Wee njoo tu"
Sabrina akasogea hadi alipo Fredy na kukaa huku mapigo yake ya moyo yakienda
kwa kasi sana, hata Fredy aligundua hiko kitu kutoka kwa Sabrina.
Fredy akainuka na kwenda mlangoni kisha akafunga vizuri ule mlango kwa funguo
na kurudi kukaa karibu na Sabrina, kila alipomsogelea ndivyo mapigo ya moyo ya
Sabrina yalivyozidi kwenda kwa kasi ya ajabu.
Fredy akainua mkono wake na kumshika Sabrina kwenye kifua chake, karibia na
mapigo ya moyo.
"Mbona moyo wako unadundadunda sana?"
Sabrina hakujibu chochote zaidi ya kumtazama tu Fredy.
Kisha Fredy akajilaza tena chali na kumwambia Sabrina
"Jilaze kama mimi"
Sabrina bila kubisha nae akajilaza chali, halafu Fredy akakaa na kumfunua
Sabrina blauzi yake na kuanza kushika kiuno chake, Sabrina alijihisi kusisimka
mwili mzima kwavile alivyokuwa akishikwa.
Gafla Fredy aliacha kumshika Sabrina na kumuuliza
"Kamba yako ya kiunoni iko wapi?"
Sabrina akashtuka baada ya kugundua kwamba Fredy anakumbukumbu juu ya ile kamba
ya kiunoni mwake.
Sabrina alikaa na kumuangalia Fredy kisha akamjibu
"Sijui"
Fredy nae akamwambia Sabrina
"Ila mi najua"
Kisha Fredy akajilaza chali na kumwambia tena Sabrina
"Nifanye kama nilivyokufanya wewe"
Sabrina akaogopa, ila akajaribu na kumfunua shati Fredy.
Hapo Sabrina alishtuka sana kwani ile kamba ilionekana kwenye kiuno cha Fredy.
Ila kabla Sabrina hajafanya chochote cha zaidi, yule bibi ambaye alimfunga
kamba hiyo Sabrina alitokea mbele yao.
Ila kabla Sabrina hajafanya chochote cha zaidi, yule
bibi ambaye alimfunga kamba hiyo Sabrina alitokea
mbele yao.
Sabrina akashtuka sana kumuona yule bibi sababu alishakufa kwa muda mrefu.
Muda huo, Fredy alikuwa kama mtu aliyepitiwa na usingizi mzito kwani alikuwa
hadi akikoroma kwa muda mfupi tu.
Yule bibi alikuwa akimtazama tu Sabrina, kisha akainua mkono wake na kunyoosha
kidole chake mpaka kwenye kiuno cha Fredy kisha ile kamba ikatoka kwenye kiuno
cha Fredy na kuhamia kwenye kiuno cha Sabrina.
Muda huo Sabrina alijikuta akiongea kwa nguvu
"Naomba unitoe hii kamba"
Yule bibi akajibu,
"Siwezi kukutoa kwani ukiitoa hiyo kamba utateseka sana kama usiku wa
jana. Ila kuna sharti moja sikukupa"
"Lipi hilo?"
"Hutakiwi kukutana kimwili na kijana yoyote yule"
Kisha yule bibi akatoweka na kumfanya Sabrina ashtuke sana.
Sabrina akajishika kiunoni na kujikuta na ile kamba ambayo hakuitaka siku zote.
Akamuangalia Fredy pale kitandani ambaye aliamka na kuwa kama mtu anayeshangaa
kisha akamuuliza Sabrina
"Kwani kimetokea nini Sabrina?"
"Sijui na siwezi kuelezea"
Sabrina akatoka nje na kuondoka kwavile hakujielewa kabisa, hakuielewa akili
yake kabisa.
Inaendeleaah
(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA
KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
No comments: