Simulizi: Je Haya Ni Mapenzi Sehemu Ya Nane (8)

Alipofika kwao, alimkuta
mama yake akiongea na Sakina.
Akawasalimia, kisha akataka kumuuliza kuhusu kutokupatikana kwake ila alijiona
akisita kuongea chochote, na badala yake akajikuta akiamua kwenda chumbani
kwake tu.
Fredy akiwa kwenye kile chumba cha kulala wageni bado alijishangaa na kujiuliza
maswali mengi bila ya majibu yoyote, akakumbuka maneno ya bibi yao alipokuwa
akimwambia Francis kuwa yule Sabrina sio mwanamke wa kuwa naye
"Inawezekana bibi aliongea maneno ya ukweli, najuta kumfahamu huyu
mwanamke kwakweli ingawa moyo wangu bado unampenda sana"
Fredy aliinuka naye na kutoka kwenye kile chumba walichokuwa na Sabrina.
Wakati Fredy anaondoka, akashangaa gafla akiitwa na yule muhudumu wa ile nyumba
ya kulala wageni
"Kaka samahani, nakuomba mara moja"
Ikabidi Fredy arudi na kusikiliza wanachomuitia.
Alipofika karibu, yule muhudumu alikuwa amebeba mkoba wa kike na kumkabidhi
Fredy
"Mmesahau mkoba wenu kaka"
Fredy akauangalia kwa makini na kugundua kuwa ule ni mkoba wa Sabrina,
hivyobasi akauchukua na kwenda nao kwao ili ajipange siku ya kuupeleka huo
mkoba kwa muhusika.
"Nitampelekea kesho huu mkoba"
Ila Fredy hakuelewa imekuwaje hadi Sabrina asahau mkoba wako.
Sabrina alipokuwa chumbani kwake, akakumbuka kuhusu mkoba wake na kuamua
kumpigia simu Fredy ili kujua kama aliuacha kule au ni vipi.
"Fredy, eti niliacha mkoba wangu kule"
"Ndio, ila nitakuletea kesho Sabrina usijari"
"Naomba unitunzie Fredy, huo mkoba ni wa muhimu sana kwangu"
"Usijali Sabrina nitautunza"
Walipomaliza mazungumzo, bibi yake Fredy alikuwa pembeni na alisikia kila kitu
ambacho Fredy alikuwa akikizungumza.
"Mkoaa gani huo Fredy?"
"Ni mkoba wa Sabrina, kuna mahali aliusahau"
"Basi nipe mie niutunze mpaka hiyo kesho kwamaana nyie wanaume huwa hampo
makini sana"
Fredy akampa bibi yake ule mkoba na kuondoka.
Sabrina hakujisikia hata kula kwa siku hiyo zaidi ya kulala tu ili aweze
kupunguza mawazo aliyokuwa nayo juu ya mambo yaliyomtokea na kile alichoambiwa
na na yule bibi alipowatokea.
Muda mwingi taswira ya yule bibi ilicheza katika akili yake, akatamani hata
siku zirudishwe nyuma ili iwe ile siku aliyopelekwa kwa yule bibi na kufungwa
kamba kiunoni ili aweze kuikataa siku hiyo katika maisha yake. Ila kama ilivyo,
maji yakishamwagika hayazoleki. Siku nayo ikipita imepita, ndiyo iliyomtesa
katika maisha yake ya sasa.
Usingizi ulimpata kwa shida sana kwani muda mwingi alikuwa na mawazo.
Kulipokucha, Sabrina alikuwa wa kwanza kuamka katika nyumba yao na moja kwa
moja alienda kukaa sebleni na kujiinamia kwa mawazo aliyokuwa nayo.
Mama yake alimkuta na kujaribu kumuuliza tena
"Una tatizo gani mwanangu?"
"Sina tatizo mama"
"Hivi kwanini huwa hutaki kusema? Unajua kukaa na mawazo sana ni dhambi?
Kwanini hutaki kuniambia mama yako ili niweze kukushauri mwanangu jamani!"
Sabrina alimuangalia mama yake kwa huruma, huku akitamani kumwambia ukweli wa
mambo ila mara zote alihisi kama atasema ukweli basi mama yake anaweza
kumfikiria kwa mabaya.
Bibi yao na wakina Fredy, alimuita Francis na kumwambia
"Mkoba huu ni wa Sabrina"
"Umeutoa wapi bibi?"
"Alikuwa nao Fredy, kuna mahali Sabrina aliusahau. Sasa mimi nataka wewe
ndio ukampelekee Sabrina"
"Kwanini mimi bibi? Na mbona umemjua Sabrina kiasi hicho wakati ulimuona
mara moja tu tena ukiwa mgonjwa!"
"Wewe mpelekee huu mkoba, ukirudi nitakwambia kila kitu. Ila ufate
nitakacho kwambia wakati unaenda"
Francis akakubali, kwani cdo alikuwa anampenda Sabrina ingawa mara ya mwisho
alimfukuza kama mbwa na ubaya ni kwamba hakujua chochote kilichoendelea kati ya
Fredy na Sabrina.
Hakujua kama walifahamiana zaidi kwa siku zote hizi ambazo yeye ameshindwa
kuwasiliana na Sabrina.
Francis alijiandaa na kuianza safari ya kwenda kwa wakina Sabrina kwa lengo la
kumpelekea ule mkoba na vilevile kwa lengo la kumuona kuwa anaendeleaje ingawa
alishaambiwa na bibi yake kuwa mwanamke huyo hafai kuwa naye, na ndiomana
Francis huwa anamshangaa bibi yake kuwa anamjua vipi Sabrina.
Francis alienda mpaka kwakina Sabrina, na mtu wa kwanza kuonana naye ilikuwa ni
mama wa Sabrina.
Alishangaa kuona yule mama akimkumbuka
"Khee mbona ulipotea wewe kijana?"
"Majukumu mama, je Sabrina nimemkuta?"
"Yupo ndani ndio, ngoja nikuitie"
Joy alimuita binti yake, na moja kwa moja Sabrina akatoka nje ili tu kujua ni
kwanini anaitwa.
Sabrina akashangaa kumuona Francis mbele ya macho yake, akajikuta akitamani
kumkumbatia.
Wakati yeye akitamani hivyo, hata Francis naye alikuwa akitamani hivyo hivyo na
kujikuta wamekaribiana na kukumbatiana, kisha maongezi mengine yakaendelea
"Nimekuletea mkoba wako Sabrina"
Sabrina akashtuka kwani hakujua kama Fredy angempa Francis ule mkoba aulete.
Francis alimpa Sabrina mkoba ukiwa ndani ya mfuko wa plastick, Sabrina alipokea
na kumshukuru Francis
"Asante sana"
"Ila unajua nilipoutoa?"
Sabrina alinyamaza kimya kwa muda, kisha akamjibu
"Sijui, niambie umeutoa wapi?"
Francis akacheka na kusema
"Najua unanizuga tu hapa, ngoja niende ila badae nitakutafuta Sabrina nina
shida sana na wewe"
"Poa, hakuna tatizo karibu sana"
Kisha wakaagana na Francis akaondoka.
Sabrina alienda chumbani kwake na kuweka ule mkoba, mawazo yakamuhama sasa.
Yakahamia kwa Francis, alijiona wazi akimpenda Francis zaidi ya alivyojihisi
kumpenda Fredy.
Alikaa na kujiuliza,
"Hivi ni nani nimpendaye kati ya Francis na Fredy? Inawezekana hawa ni
ndugu, itakuwaje sasa? Ila kama Francis akiamua kuwa na mimi tena basi ni bora
nikawa mbali na Fredy kwavile Fredy alishanikuta nikiwa na mahusiano na Francis
tayari."
Mapenzi yalionekana kumchanganya sasa baina ya watu hawa wawili, ila kila
alipoikumbuka ile sauti ya yule bibi kuwa haruhusiwi kulala na mwanaume yeyote
yule, alinyong'onyea.
Jioni ya siku hiyo alienda mahali na kukutana na Francis ambaye alimuomba
msamaha kwa yale aliyomwambia.
"Nisamehe Sabrina, bado nakupenda"
"Hata na mimi nisamehe, kwani bado nakupenda"
Wakakumbatiana kwa furaha bila ya kujali ni kwanini waligombana.
Kisha wakaagana huku wakiwa na nyuso za furaha, ambazo zimejaa mapenzi.
Sabrina alirudi nyumbani kwao, alipofika nje alikutana na mama yake
aliyemwambia
"Tena afadhari, kuna mgeni wako ndani huko"
"Mgeni gani? Kwani baba yupo?"
"Baba yako hayupo, kasafiri tena ila kwavile wewe una mambo mengi
akashindwa kukuaga. Kuhusu mgeni, ingia mwenyewe ndani utamuona"
Sabrina alisononeka kuona baba yake ameondoka bila ya kumuaga, kwahiyo akaingia
ndani kwa msononeko.
Akamkuta Fredy akiwa ndani kwao, na kumshangaa
"Kheee Fredy!"
"Nini sasa Sabrina jamani!"
"Huogopi kuja kwetu bila taarifa?"
"Niogope nini kwa mkwe wangu?"
Sabrina akamuangalia tu Fredy, kisha akamfata alipokaa.
Akatamani kumwambia ukweli kuhusu yeye na Francis, ila alishindwa kwani alijua
lazima Fredy angejisikia vibaya.
"Sabrina, unafanya mambo mengi sana yasiyoeleweka. Ila mi sijali sababu
nakupenda sana Sabrina, jana uliondoka bila hata ya kuniaga hadi ukasahau mkoba
wako mule ndani. Ila kwa mapenzi yangu, nikauchukua na kwenda kukutunzia
nyumbani....."
Sabrina akamkatisha Fredy hapo na kumwambia
"Na kwa mapenzi yako, ukaamua kumpa Francis aniletee"
Fredy akashangaa sana, ila akili yake ikamwambia kuwa ni bibi yao tu ndio
aliyefanya hivyo.
"Kwahiyo, Francis ndiye aliyekuletea mkoba?"
"Inamaana hujui au?"
"Sijui ndio"
"Hebu niambie kwanza, je kuna undugu kati yako wewe na Francis?"
"Hayo nitakwambia tu, ila naomba uniletee huo mkoba wako mara moja
nione"
Sabrina hakusita, moja kwa moja akaenda chumbani kwake kwa lengo la kuutoa ule
mkoba ili akampe Fredy aweze kuuona.
Francis nae aliporudi kwao ile jioni, moja kwa moja bibi yake alimuita na
kumuuliza
"Ule mkoba uliufikisha kwa Sabrina?"
"Ndio bibi"
"Hukuufungua kweli wewe!"
"Siwezi kufanya kitu ambacho umenikataza tayari, siwezi kabisa bibi yangu.
Ila nimerudiana na Sabrina"
"Kwanini umerudiana nae? Yani ndio hapo unaponikera wewe mtoto"
"Bibi, nampenda sana Sabrina. Alikosea ndio ila nimemsamehe, nampenda
kwakweli"
"Hakuna shida, je unaweza kuwa na mahusiano na mwanamke asiyeona?"
"Kivipi bibi?"
"Namaanisha kipofu"
"Mmmh! Mie sitaki mwanamke asiyeona bibi, na ndiomana nikampenda
Sabrina"
"Kwasababu anaona, si ndio!"
"Ndio bibi, na macho yake yanavutia sana"
"Ila weka akilini jambo hili, hata binadamu anayeona anaweza kuwa kipofu
kwa sekunde chache tu"
"Mbona sijakuelewa bibi?"
"Ndiomana nikakutuma wewe, kwavile ningemtuma Fredy angeharibu kila kitu
yule na huwa hajielewi kabisa"
"Kwani angefanyaje?"
"Angechungulia ule mkoba wa Sabrina"
"Kwani ulikuwa na nini?"
"Ulikuwa na vitu vya kike ambavyo hairuhusiwi mwanaume kuviona. Usipende
sana kudadisi mambo, unaweza ukawa kichaa bure"
Francis alichukua muda mrefu kuyatafakari maneno ya bibi yake bila ya jibu la
aina yoyote ile.
Mwisho wa siku aliacha kama mambo yalivyo na kuendelea na mambo yake mengine.
Sabrina, alichukua ule mkoba wake na kwenda kumpa Fredy.
"Kheee ndio alikuwekea kwenye rambo kabisa!"
"Ndio, hivyo hivyo alivyouleta"
Fredy akautoa ule mkoba kwenye rambo na kuupakata, kisha akataka kuufungua.
Sabrina akamzuia,
"Sasa unataka kitu gani humo Fredy?"
"Lazima nione, labda Francis kakuwekea vibarua vyake humu"
"Mmmh Fredy acha wivu bhana"
"Siwezi hadi nione kilichopo ndani"
Ikabidi Sabrina amuachie Fredy ule mkoba aangalie sababu alijua wazi kuwa
hakuna chochote cha ajabu kwenye mkoba wake.
Fredy akafungua ule mkoba, kikatoka kitu kama moshi na kuyakumbuka macho ya
Fredy.
Fredy akaachia ule mkoba na kupiga ukelele wa nguvu kisha akaanguka chini.
Fredy akafungua ule mkoba, kikatoka kitu kama
moshi na kuyakumba macho ya Fredy.
Fredy akaachia ule mkoba na kupiga ukelele wa
nguvu kisha akaanguka chini.
Sabrina akamuita mama yake aliyekuja mbio sana kutokana na ile kelele
aliyoisikia kutoka ndani kwake.
Alipoingia alishangaa kumuona Fredy akiwa chini
"Imekuwaje Sabrina?"
"Sijui mama, ni gafla tu"
Mama huyu akaenda kuleta maji na kuanza kumwagia Fredy, hadi Fredy akazinduka.
Ila alipozinduka, alikuwa akifikicha macho yake na kudai kuwa yanamuwasha sana.
Joyce alichukua yale maji na kujaribu kumnawisha Fredy kwenye macho, lakini
bado Fredy alilalamika kuwa macho yanamuwasha tena sana tu.
Aliyafikicha kwa muda, huku nao wakijaribu kuendelea kumpa huduma ya kwanza
ambayo kwao ilikuwa ni kumuosha kwa maji.
Baada ya muda kidogo, muwasho ulipungua kwenye macho ya Fredy, naye akajaribu
kuyafumbua ili aone lakini hakuona kitu chochote kile.
"Jamani sioni, sioni jamani"
Wakajaribu kufanya kila kitu walichoweza lakini bado Fredy aliendelea
kulalamika kuwa hawezi kuona chochote.
Joyce aliamua kumbembeleza Fredy ili atulie na wajue cha kufanya kwa wakati
huo.
Fredy akatulia kiasi na kumpa mama Sabrina nafasi ya kuongea
"Kwani imekuwaje Sabrina?"
"Hata mi mwenyewe sielewi mama, yani nashangaa tu hapa"
"Hebu nipe mlolongo mzuri wa matukio nikuelewe"
Sabrina akamwambia mama yake kuhusu ilivyokuwa muda mfupi uliopita.
"Mbona sielewi? Kwani hiyo pochi ina nini?"
"Haina kitu mama"
Kisha Sabrina akachukua ile pochi na kubwaga vyote vilivyokuwemo ndani yake.
"Si unaona mwenyewe mama, hii pochi haina chochote yani hata mi mwenyewe
nimeshangaa tu hapa"
"Mmh makubwa haya mwanangu"
Wakaanza kujadiliana jinsi ya kumrudisha Fredy kwao na jinsi ya kuwataarifu
ndugu zake kuhusu yaliyotokea.
Basi Joy akainuka na kumuacha mwanae Sabrina ili amuulize vizuri namna
watakavyomrudisha kwao.
"Kwakweli Fredy mi nimechanganyikiwa hapa, sasa tutakupelekaje
kwenu?"
"Mpigie simu Francis ili aje kunichukua"
Sabrina akakubaliana na hilo kwa Fredy, kisha akaenda kumwambia mama yake
ambaye pia aliafikiana kuhusu hilo na kuamua kumpigia simu Francis ili aje
kumfata ndugu yake.
"Kwani kuna nini Sabrina?"
"Njoo tu utaona hukuhuku, tafadhari njoo upesi"
Ingawa Francis hakujua anaitiwa kitu gani ila ile kauli ya kumwambia aende
upesi ilimpa wasiwasi na kumfanya ajiandae haraka na kuianza safari.
Francis alipofika kwakina Sabrina, alikaribishwa ndani na kushangaa kumuona
Fredy akiwa pale ndani.
Moja kwa moja Francis akauliza
"Vipi jamani!"
Fredy akajibu,
"Sioni Francis, sioni mwenzio"
"Imekuwaje kwani Fredy?"
"Nipeleke nyumbani tafadhari, nitakueleza tukifika nyumbani"
Ikabidi Francis asaidiane na Sabrina katika kumpeleka Fredy nyumbani kwao.
Walipofika, walimpeleka Fredy chumbani akapumzike.
Ikabidi Sabrina amuage Fredy,
"Tafadhari usiniache Sabrina"
"Usijali Fredy, sitakuacha kamwe"
"Nakupenda sana Sabrina, tena sana"
Kisha Francis akamfata Sabrina kuwa watoke ili amsindikize.
Francis akamsikia Fredy akimwambia Sabrina
"Tafadhari Sabrina, nibusu kabla hujaenda"
Sabrina akainama na kumbusu Fredy, kisha akamuaga na kutoka nje na Francis.
Ila kile kitendo cha Sabrina kumbusu Fredy kilimuumiza sana na kujikuta
akipatwa na wivu juu yao.
Walipotoka nje akamuuliza
"Kwani kuna nini kinaendelea kati yako na Fredy?"
Sabrina alishindwa kujibu kwavile hakuelewa ni kitu gani atamwambia Francis ili
aweze kumuelewa.
"Naomba umuulize Fredy mwenyewe"
"Niambie vizuri Sabrina, si unajua kama nakupenda! Halafu Fredy ni ndugu
yangu, ila kwanini unataka kunifanyia hivi Sabrina?"
Sabrina hakuwa na jibu na akajua wazi kama ataendelea kuongea kuhusu hilo na
Francis basi lazima kuna ugomvi utatokea tu, hivyobasi alipoona gari inapita
alisimamisha na kupanda ili tu kuweza kuepukana na marumbano na Francis
ukizingatia usiku ulishakuwa mkubwa.
Sabrina akiwa kwenye lile gari, alikaa na kijana mmoja aliyemsikia kwa jina
moja ambalo wenzie walikuwa wakimuita.
Kijana huyo alikuwa akiongea sana kwenye lile gari, na kila alipoongea aliwafurahisha
watu wengi akiwemo na yeye mwenyewe Sabrina.
Na walipofika kwenye kituo, Sabrina alijikuta akishuka pamoja na yule kaka.
Ikabidi amuongeleshe tu,
"John!"
"Kheee dada umenijuaje?"
"Nimesikia watu wakikuita hivyo kwenye gari, nimeyapenda sana maongezi
yako"
"Kumbe eeh! Nipe namba zako basi"
Sabrina hakuona tatizo kumpa huyu kijana namba zake ili waweze kujadiliana
zaidi na zaidi.
Kisha wakaagana na kuondoka.
Sabrina alipofika nyumbani kwao alimsikia mama yake akifanya maombi, haswaa
alimsikia akimuombea pia na yeye kuwa arudi salama.
Alikaa pale nje na kumsikiliza mama yake kwa makini zaidi hadi alipomaliza yale
maombi ndipo naye akaingia ndani.
"Sabrina, mgonjwa anaendeleaje?"
"Nimemuacha pale kwao amelala mama"
"Amegoma tena kuhusu hospitali?"
"Amekataa kabisa, anaamini kuwa atapona tu"
"Ndio, Mungu mkubwa hata mi naamini kuwa atapona tu"
"Basi vizuri mama, ngoja niende chumbani kwangu"
Sabrina aliingia chumbani kwake, ila kabla hajafanya chochote alipigiwa simu na
yule John aliyekutana nae kwenye basi.
"Hivi jina lako unaitwa nani?"
"Naitwa Sabrina"
Basi John akaanza kumwambia Sabrina vitu vingi vya masikhara na kumfanya
Sabrina acheke sana kutokana na kile ambacho John alikuwa anamwambia hadi pale
alipokata simu, Sabrina alikuwa ameshacheka sana hadi machozi yakamtoka kwa
kucheka na kujikuta akiongea peke yake
"Yani huyu kijana ana vituko sana dah, nimecheka hadi raha"
Kisha akaenda kuoga na kurudi kulala.
Akiwa usingizini, akamuona yule bibi wa wakina Francis akiwa ameushika ule
mkoba wake aliousahau katika nyumba ya kulala wageni.
Kisha akaifungua na kuweka vitu vyenye asili ya ungaunga halafu akawa kama
ananenea vitu fulani kwenye ule mkoba.
Kisha Sabrina akajiona akishika ule mkoba, vikatoka vitu kama moshi kwenye ule
mkoba na kuelekea kwenye macho yake, kisha akahisi macho yakimuwasha sana na
alipokuja kufumbua alikuwa ni kipofu tayari.
Sabrina akanza kulia bila ya kujua kama anaota, hadi mama yake akakimbilia
chumbani kwa Sabrina huku akijua kuwa binti yake kapatwa na matatizo.
Alimkuta akiwa kalala chali huku machozi yakimbubujika
"Wee Sabrina, wee Sabrina"
Sabrina akashtuka na kujifikicha macho,
"Una matatizo gani wewe mtoto?"
"Kumbe naona mama!"
"Kwani ulikuwa huoni! Mbona una mambo ya ajabu wewe mtoto?"
Alitafakari ndio akagundua kwamba alikuwa anaota.
"Samahani mama, ni ndoto tu"
"Aaah! Una kichaa sana wewe mtoto wangu, muone na akili zake zilivyofupi.
Ngoja nikamalizie usingizi wangu mie"
Akatoka na kwenda chumbani kwake huku akijisemea
"Najuta kumpa mwanangu jina la shangazi yake"
Kulipokucha, Sabrina akaamka na mawazo mapya kichwani mwake kwani ile ndoto
aliona kama vile imempa mjibu ya maswali kadhaa katika akili yake.
"Inawezekana ule mkoba wangu ulifika kwa yule bibi na ndiomana nimeletewa
na Francis, ni lazima yule bibi alifanya kitu kibaya kwenye ule mkoba ili aweze
kunidhuru mimi, sasa kamdhuru mjukuu wake mwenyewe! Mmh sijui itakuwaje sasa.
Inamaana Fredy kawa kipofu badala yangu! Lazima nifanye kitu cha
kumsaidia"
Sabrina alijiona kuwa yupo njiapanda kwasasa na haya mambo kwani hakuyatarajia.
Mchana wake alienda kwa Sakina, alikuwa na mengi ya kumueleza ukizingatia ni
siku kadhaa zimepita bila ya wao kuongea chochote.
"Bora umekuja Sabrina mdogo wangu"
"Kuna nini dada?"
"Nina khabari mbaya kuhusu hiyo kamba yako ya kiunoni"
"Mmh! Hebu niambie vizuri dada, maana hata sielewi kitu hapa."
"Ni hivi, mimi niliondoka hapa kwenda kuulizia kuhusu hiyo kamba yako kwa
watu wenye uzoefu nazo"
"Eeh wamesemaje?"
"Ni hivi mdogo wangu, kwavile aliyekufunga hiyo kamba alishakufa na hakuna
wa kukufungua tena basi lazima wewe uliyefungwa hiyo kamba upate madhara"
"Mmh yapi hayo, niambie dada jamani"
Huku moyo wa Sabrina ukienda kwa kasi sana, Sakina aliendelea kumueleza
"Kwanza kabisa, hutakiwi kukutana kimwili na mwanaume yoyote yule.
Hairuhusiwi mwanaume yoyote kuiona hiyo kamba yako, na siku ile yule mkaka
aliamka ni kwa bahati tu. Pia, hiyo kamba haitakiwi kukatwa na mtu yeyote yule
labda kama itatokea siku ikakatika yenyewe huo ndio utakuwa uzima "
"Jamani dada, naishije mimi sasa kwa mtindo huo? Kwahiyo sitakiwi kuwa na
mchumba? Kwahiyo mimi sitaolewa wala kuwa na watoto?"
"Ndio hivyo Sabrina, kwahiyo kuwa makini sana. Na ikitokea mtu akakukata
hiyo kamba jua kwamba mtu huyo atapata madhara makubwa sana, vilevile kila
mwanaume utakayelala nae atakufa na ukibeba mimba lazima itatoka"
Sabrina aliogopa sana na kutetemeka huku machozi yakimtoka, hakutaka kuwa na
hali ya namna hiyo katika maisha yake kwani alipenda kuwa kama wanawake wengine
duniani.
"Sasa nitafanyaje dada?"
"Cha msingi ni kuombea hiyo kamba ikatike yenyewe ili uwe huru"
"Itabidi niende tena kwenye lile kaburi la yule bibi ili nimuombe
anipunguzie adhabu hii au hata aikate kimiujiza"
"Labda tufanye hivyo mdogo wangu, basi kesho asubuhi na mapema twende
huko"
"Sawa dada"
"Ila kuwa makini sana na hiyo kamba, jihadhari mtu yeyote asije akaiona
hiyo kamba Sabrina. Sawa eeh!"
"Hata hivyo nipo makini sana, hata mama tu ndani kwetu hajui kama nipo
hivi"
Sabrina akakubaliana na Sakina juu ya mpango wao wa siku ya kesho wa kwenda
kwenye kaburi la yule bibi.
Sabrina alirudi nyumbani kwao akiwa amepunguza kiasi kidogo cha mawazo na
kuongeza kiasi kingine ambacho hakujua kitaishia wapi.
Hakujua hatma yake na ile kamba yake ya kiunoni, kwavile alikuwa na mawazo
mengi sana, akama ni vyema ampigie simu yule John mwenye vituko ili aweze
kucheka na kufurahi.
Akaipiga ile simu, ila haikupokelewa na John kama alivyotarajia bali
ilipokelewa na sauti ya kike
"Samahani, John yupo?"
"Unamuulizia John wewe kama nani?"
Sabrina akaona kuwa itazuka shari pale na kuamua kukata ile simu huku
akijisemea
"Kumbe huyu John ana mwanamke, kwanini hakuniambia sasa?"
Alihisi kama moyo ukimuuma vile na kujigundua kuwa ameingiliwa na mdudu wivu
kwa John wakati si mpenzi wake.
"Ngoja niachane na mawazo ya kijinga ilihali najua wazi kwamba siwezi kuwa
na mpenzi kutokana na matatizo niliyonayo, hata najishangaa kuwa naanzaje
kupenda jamani"
Hali ya kuwa hivi ilimsumbua sana Sabrina na kujikuta akitamani kesho yake
ifike na waweze kwenda huko makaburini na pengine ukawa ndio ukombozi wake
kwenye maisha.
Usiku wa siku hiyo alikuwa akiwaza tu kuhusu kamba yake ya kiunoni
"Ni kweli inanisaidia kuona wachawi, na pia inanisaidia kupambana nao
lakini kwanini initese hivi!! Na mbona kabla sijawa nayo hao wachawi
hawakunisumbua?"
Alikuwa akiwaza tu muda wote huku akiamini kwamba akienda kule makaburini kulia
na kumuomba yule bibi basi atasalimika na kusahau kwamba ameshawahi kufanya
hivyo kabla lakini tatizo bado liliendelea tena kwa makubwa zaidi kila kukicha.
Usingizi ulimpitia akiwa bado na mawazo.
Wakati yupo usingizini, alikuja yule mmama waliyekutana nae mchana. Kama
kawaida Sabrina alishtuka na kuanza kuangaliana nae,
"Kwani mnataka nini kwangu nyie?"
"Tunataka uwe mshirika mwenzetu"
"Sitaki, na muondoke"
"Nimekuja peke yangu leo, sina nia mbaya ila nataka uwe mshirika
mwenzetu"
Sabrina akainuka huku akitetemeka, akachukua maji yaliyokuwepo pembeni yake na
kumwagia yule mchawi, muda huo huo yule mchawi akatoweka.
Sabrina akashangaa kuona kuwa hata maji nayo ni dawa, ila hakuweza kulala tena
hadi palipokucha.
Aliamka na kwenda kuoga ili kujiandaa kwaajili ya safari aliyopanga na Sakina.
Wakati anaanza kujiandaa tu, mama yake akaingia gafla chumbani kwake bila ya
hodi na moja kwa moja alimshangaa Sabrina kiunoni
"Nini hiko cheusi kwenye kiuno chako Sabrina?"
Sabrina akashtuka sana na kuchukua khanga ili kujifunika.
Kama kawaida ya Joy, hakutaka kukubaliana na kujifunika kwa mwanae.
Hivyo basi akamfata na kuitoa ile khanga kwa nguvu,
"Khee una kamba kiunoni Sabrina! Tena nyeusi! Mambo gani hayo ya
kishirikina Unayaleta ndani kwangu!"
Akamfata karibu, kisha akachukua mkasi uliokuwepo kwenye meza ya Sabrina na
kuikata ile kamba.
Inaendeleeah
(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA
KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
No comments: