Wakonta: Daktari Kaniambia Naweza Kutembea
MUNGU mkubwa! Ndivyo unavyoweza kutamka kutokana na daktari kueleza kuwa binti mrembo, Wakonta Kapunda ambaye ni mlemavu aliyepooza kiwiliwili yaani kuanzia mabegani mpaka miguuni, anaweza kutembea tena.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Ijumaa Wikienda, akiwa nyumbani kwake Kigamboni, Dar, Wakonta alisema anamshukuru Mungu kwani kwa sasa ameanza kupata hisia kwa mbali.
Mwanadada huyo aliendelea kusema kuwa daktari wake alimhakikishia kwamba kutokana na mazoezi anayoyafanya, ipo siku ataamka na kujikuta yupo kawaida kama alivyokuwa mwanzo kabla hajapata ajali yaani anatembea vizuri na viungo vyake vyote vinafanya kazi.
“Sasa hivi nimeanza kupata hisia kwa mbali kitu ambacho kinanipa matumaini sana kama alivyoniambia daktari kuwa ipo siku nitaweza kuamka na kutembea tena, halafu hali yangu ikawa imerudi kama zamani,” alisema Wakonta.
Wakonta ambaye kwa sasa amenunua gari lake maalum kwa ajili ya watu wenye tatizo kama lake lenye thamani ya shilingi milioni 12, alisema amelinunua kwa sababu anajipenda na hajawahi kukata tamaa.
“Sijawahi kukata tamaa hata kidogo na wala sifikirii kufanya hivyo kwa sababu nimeshajikubali na hali yangu niliyonayo ndiyo maana kila kitu kwangu kinaenda sawa,” alisema Wakonta.
Mwaka 2012, Wakonta alipata ulemavu alipokuwa kwenye mahafali ya kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Wasichana ya Korogwe jijini Tanga baada ya mwanafunzi mwenzake kupanda kwenye gari na kuendesha kisha kurudi nyuma kwa nguvu na kugonga wanafunzi mbalimbali akiwemo na yeye.
Mwanafunzi aliyedaiwa kuwasha gari na kusababisha ajali hiyo, alijulikana kwa jina la Kibibi. Mbali na Wakonta, wengine waliokumbwa na ajali hiyo ni Zahra Jumanne (19), Renata Renatus (25), Sophia Godfrey (19), Victoria Mtwale (19), Nancy James (19) na Mwanamkonda Kapunda (19) ambao wote walikuwa kidato cha sita mwaka huo.
KUTOKA KWA IJUMAA WIKIENDA
Ni jambo jema kwa binadamu yeyote kutokata tamaa hata kama anapitia magumu kiasi gani. Pongezi kwako Wakonta kwa kutokata tamaa na changamoto zote unazopitia, wewe ni mfano wa kuigwa, kikubwa tunakuombea ili siku moja urudi katika hali yako ya kawaida.
STORI: IMELDA MTEMA, DAR
(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA
KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
No comments: