Ni sahihi kuoana kwa sababu ya UJAUZITO?
WEWE ni mwerevu kwa kuchagua kusoma ukurasa huu. Nakuhakikishia uamuzi wako ni sahihi kwa sababu baada ya hapa, utakuwa umeongeza kitu kikubwa sana kichwani mwako. Itakuwa bora zaidi kwa yule ambaye atakuwa amejifunza, kuhifadhi na kufanyia kazi yale ambayo ameyasoma hapa. Naendelea na mada yetu tunayojadili kuhusu suala la ujauzito. Mengi tuliona wiki iliyopita, leo tunaendelea katika hatua nyingine.
MUHIMU KUJUA
Rafiki zangu wapendwa, kama tulivyoona katika vipengele vilivyopita kwenye toleo la wiki jana, suala la kupata mimba kabla ya ndoa (hasa kwa wale ambao hawaishi pamoja) si sahihi na ni jambo la hatari. Kupata mimba kabla ya ndoa, hakukubaliki katika imani yoyote ya dini, bila shaka hata Wapagani hawaruhusu jambo hili. Wakati tunapoendelea kujadili kuhusu mada hii, lazima utambue kwamba utakuwa upo kwenye makosa na dhambi kwa kufanya kitu kilicho kinyume na maadili ya imani unayoabudu.
Najua wengi hawapendi kusikia jambo hili, lakini ndiyo ukweli wenyewe. Si sahihi kukutana kimwili kabla ya ndoa. Sisemi haya nikimaanisha labda mimi ni msafi sana, la hasha! Huenda nami kuna mahali niliwahi kuteleza, lakini hapa tujadili namna ya kushughulikia tatizo hili na maisha yaendelee yakiwa kwenye furaha tele. Twende tukaone zaidi…
MIMBA KABLA YA NDOA
Je, wewe unayesoma hapa umepata mimba kabla ya ndoa na unahaha namna maisha yako yatakavyokuwa baada ya tukio hilo? Je, unafikiria jinsi utakavyoishi na familia yako ukiwa na ujauzito? Ni kweli ni magumu kidogo kwa maisha ya kawaida ya kibinadamu lakini kwa kuwa memba wa safu hii, utakuwa mwenye ufahamu na utajua namna ya kukabiliana na changamoto hiyo huku maisha yako yakiendelea kuwa ya amani na furaha tele.
(i) Hatua ya kwanza
Mshirikishe mwenzako. Kama una uhakika kuwa mimba uliyonayo ni ya mhusika wako, mweleze ukweli. Tafuta muda mzuri, mwite na umjulishe juu ya ‘bahati’ mbaya iliyotokea. Hakikisha katika hatua hii, huoneshi kuwa umekutana na tatizo kubwa katika maisha yako. Aone unazungumza juu ya ‘baraka’ ingawa imekuja kwa muda ambao si sahihi. Usioneshe matarajio yoyote katika mazungumzo yako. Kikubwa ni kumjulisha tu kuwa sasa una mimba yake!
(II) HATUA YA PILI
Katika matamshi yako usioneshe kabisa kwamba mimba hiyo ni sababu ya kukuoa na anachotakiwa kufanya ni kufunga ndoa na wewe au kuhamia kwake. Achana na vitisho kabisa.
(III) HATUA YA TATU
Acha papara, mpe nafasi ya kuzungumza. Msikilize kwa makini maoni yake. Vyovyote itakavyokuwa, maadamu una uhakika mimba ni yake kila swali lake litakuwa na jibu. Kubaliana na mawazo yake, lakini kamwe usiruhusu mawazo yake ya kwenda kutoa mimba yakaingia kichwani mwako.
(IV) HATUA YA NNE
Sasa mnatakiwa kujadiliana pamoja. Zungumza naye kuhusu athari (angalau zile za kawaida kabisa kama matatizo ya uzazi nk) za kutoa mimba. Mwache huru aamue anachotaka. Kama mnapendana na lengo lenu ni ndoa, basi hapo inaweza kuwa tiketi ya kuharakisha hilo ili kukuepusha na aibu nyumbani kwenu.
Kama atasema hayupo tayari usimng’ang’anize ila zungumza naye kuhusu utaratibu unaofaa wa kulea mimba na mtoto hapo baadaye ikiwa ni pamoja na kujitokeza nyumbani kwenu (kupitia wazee) na kueleza kuwa anahusika na mimba yako na kwamba (labda) anajipanga kwanza kabla ya kuchukua uamuzi mwingine hapo baadaye. Mada bado inaendelea, wiki ijayo tutaingia katika hatua nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano na Mapenzi. Ameandika vitabu kadhaa, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.
(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA
KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO
No comments: