JINSI YA KUJINASUA KWENYE MAUMIVU YA KUACHWA
MARA nyingi sana inapotokea umejeruhiwa penzini, hususan na mtu ambaye ulikuwa na malengo naye, ni vigumu mno kupenda tena.
Ni vigumu sana kumuamini tena mtu wa jinsia tofauti na yako. Wakati mwingine unaamini mtu wa jinsia ya tofauti na yako ni kama muuaji, ni mtu asiyestahili kuwa karibu yako. Ndugu zangu, tunakosea sana. Haya yote yanatokea kwa sababu fulani. Japo hakuna anayeyafurahia, lakini endapo yakitokea, usihuzunike moyoni mwako. Chukulia kama changamoto na amini utasimama tena.
Sahau mapito yako. Elewa kwamba aliyekutenda hilo, wakati wewe unaumia yeye hana habari na wewe. Kwa nini uumie kwa sababu yake? Kataa kuumia. Maisha mazuri kwako yapo. Amini furaha yako ipo mbeleni, itachelewa tu, lakini inakuja. Mtu sahihi yupo tu wala usiumie moyo.
Chukulia kuachwa kwako kama somo muhimu ili usirudie makosa. Ukweli ni kwamba wakati mwingine tunapaswa kuanguka ili tuweze kusimama upya. Kujifunza kutokana na makosa yako ya zamani ni njia pekee ambayo unaweza kujiongoza kupata upendo unaostahili badala ya kufanya makosa mengine tena.
Usimchukie aliyekuacha maana huwezi kujua mngeendelea naye angefanya nini juu ya maisha yako. Yawezekana angekuja kuwa tatizo huko baadaye. Yawezekana angekuja kuwa mwiba au sumu katika pendo lako wakati tayari mpo kwenye ndoa. Mpende, mruhusu aende, usimchukie. Muombee heri huko aendako. Mchukulie aliyekuumiza hakuwa mbaya isipokuwa hakuwa tu mtu bora kwako.
Jiweke kwenye wakati mzuri wa kuruhusu moyo wako upende tena. Maisha lazima yaendelee, aliyekuumiza anapenda tena huko aliko, kwa nini wewe usipende tena? Utaumia mpaka lini? Utahuzunika hadi lini? Kataa huo utumwa.
Jiamini kwamba wewe ni bora, amini kwamba kilichotokea hadi ukaachwa ni changamoto tu. Usitafute mchawi. Amini kwamba unaweza kuingia kwenye uhusiano mwingine na ukasahau kabisa maumivu uliyoyapitia.
Mapenzi siku zote ni hatari. Kumkabidhi mtu moyo wako ni jambo linalohitaji imani ya hali ya juu. Baada ya kuishi huru muda mrefu, chukua nafasi ya kumpa mtu nafasi nyingine ya kuanzisha naye uhusiano. Ruhusu moyo wako upende tena na ujifunze kutokana na uhusiano uliopitia.
Kama kuna mahali unahisi ulikosea, ni wakati wa kujirekebisha na kusimama upya. Tafuta furaha ya moyo wako. Usikubali moyo wako uishi kwenye majonzi. Hakikisha unaisaka furaha yako, upe amani moyo wako kwa kuzungumza na watu sahihi, watakaokupa furaha kila siku badala ya karaha.
Ukimpata mtu mwingine, epuka sana kumlinganisha na mpenzi wako wa zamani. Tengenezeni penzi jipya ambalo litakuwa na misingi mtakayojiwekea ninyi. Penzi zuri ni lile mnalolitengeneza wenyewe. Kila mmoja wenu amtie moyo mwenzake, pangeni mipango yenu na kuacha kabisa kukumbuka huko mlikotoka.
Cha msingi ni kuhakikisha unaingia kwenye uhusiano mpya na mtu sahihi. Mtu ambaye kweli hana makandokando, hana macho ya tamaa na kweli asiwe na mtu mwingine zaidi yako. Elezaneni ukweli juu ya misingi ya safari yenu. Kila mmoja ajue umuhimu wa penzi lenu, mjue kama kweli mnaweza kusonga mbele na mna malengo yanayofanana au la.
Kama hamna malengo yanayofanana ni vyema kukatisha safari mapema kabla hamjafika mbali. Msipotezeane muda, msome mwenzako kama ana malengo ya mbali au la. Ni matumaini yangu mtakuwa mmenisoma. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
No comments: