Sababu 9 za kwanini umsamehe aliyekukosea

 


Umesikia mara nyingi sana kuwa “Unatakiwa kusamehe na kusahau”.

Nini maana halisi ya kusamehe? Kusamehe ni kuamua kutomchukulia mtu hatua na kuondoa kinyongo moyoni mwako kutokana na jambo baya ulilofanyiwa na mtu huyo. Kusamehe kunasema hutakiwi kusikia neno “nisamehe” ndipo uendelee na maisha yako. Kusamehe kumewekwa na ni kwa manufaa zaidi kwa yule aliyekosewa.

Ni wazi kuwa katika maisha kuna kukoseana kwa namna mbalimbali. Wapo watu wasiopenda suluhu wala msamaha. Ni dhahiri kuwa ni lazima wewe uliyekosea ufahamu manufaa na sababu za kumsamehe na kumsahau aliyekukosea; manufaa hayo ni haya yafuatayo.

1. Hukuweka huru

Kutokusamehe kunakufanya ujisikie vibaya na kuwa kama mfungwa. Jambo baya ni pale utakapomwona yule aliyekukosea anafuraha na anaendelea na maisha yake bila tatizo. Kila wakati unalitafakari swala hilo na unahisi limetawala kila unachofanya. Hivyo ni vema ukasamehe ili uwe huru maishani mwako.

2. Hukuwezesha kuendelea mbele na maisha yako

Kuna mambo mengi mazuri na muhimu zaidi maishani kuliko chuki na hasira. Kwanini ufikiri tu kuhusu mtu aliyekuumiza au kukukwaza? Usipo msamehe utabaki kuumia tu na kushindwa kuendelea mbele na maisha yako.

3. Kulinda afya yako

Uchungu na maumivu uliyoyapata baada ya kukosewa ni dhahiri kuwa yanaweza kusababisha matatizo kama vile msongo wa mawazo. Ikumbukwe kuwa msongo wa mawazo ni chanzo cha maradhi mbalimbali kama vile shinikizo la damu, kiharusi n.k. Sasa kwanini usisamehe ili ulinde afya yako? Samehe sasa.

4. Huondoa hasira na chuki

Ni dhahiri chuki na hasira huingia nafsini na moyoni mwako mara mtu anapokukosea. Ukiwa na chuki na hasira moyoni au nafsini mwako ni wazi kuwa utapunguza tija katika yale unayoyafanya. Hivyo basi unaposamehe unajiweka katika hali nzuri zaidi kiutendaji.

5. Unaondoa utawala wa mtu mwingine kwenye akili yako

Naamini unafahamu jinsi unavyomkumbuka mtu aliyekukosea kila wakati akilini mwako. Ni wazi kuwa ukisikia jina au hata sauti yake tu unapata maumivu kutokana na lile alilokufanyia. Ni dhahiri huku ni kutawaliwa na mtu mwingine katika akili au fikra zako. Msamehe leo na uendelee na maisha yako yenye uhuru.

6. Utulivu wa akili

Nimeshuhudia watu wengi wakikosewa wanashindwa kupata utulivu wa akili. Jambo hili limewafanya wengi hata kushindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku. Mara kichwa kinauma, mara najisikia kukosa amani, mara sina mood n.k. ni viashiria vya kukosa utulivu wa moyo na akili. Nakushauri ipe akili yako nafasi ya kutulia kwa njia ya kusamehe waliokukosea

7. Ni aina bora ya kisasi

Je unafikiri kulipa kisasi ni kufanya baya kama ulilofanyiwa? Kama jibu ni ndiyo, unakosea kwa kiasi kikubwa. Ni dhahiri kisasi kinachouma sana ni pale mtu anapokufanyia jambo baya lakini wewe unamfanyia jema. Naamini hata kwa wale wenye imani za kidini wanakubaliana na hili.

8. Kuonyesha upendo

Kuna wakati mtu aliyekukosea anaumia kutokana na kosa alilolifanya lakini anashindwa kuja kuomba msamaha. Lakini kumsamehe kunadhirisha upendo ulio nao kwake hata kama hajaja kukuomba msamaha.

9. Kiashiria cha ukomavu

Hakuna mtu mwenye uwezo wa kusamehe kama hana ukomavu wa kiakili na hekima na busara za kutosha. Watu wachanga hupenda kubeba na kutunza chuki na hasira; wao ni heri kubaki na maumivu hata maisha yao yote kuliko kuyaachilia ili wawe huru.

Neno la Mwisho:

Ni dhahiri kusamehe ni jambo gumu; lakini ni muhimu hasa kwako wewe uliyekosewa. Ikiwa ni mpenzi, rafiki, ndugu, mazazi au hata mfanyakazi mwingine amekukosea ni vyema ukamsamehe. Kwa kusamehe kutakufungulia ukurasa mwingine mpya wa maisha na kuruhusu majeraha kupona. Kwa njia hii utafanya maisha yako kuwa yenye tija, furaha na amani zaidi.



(WAKUBWA TU 18+) JIFUNZE UFUNDI NA UTUNDU KATIKA MAPENZI UBORESHE MAHUSIANO YAKO PAKUA APP YA UFUNDI CHUMBANI , BONYEZA HAPA KUIDOWNLOAD KWENYE SIMU YAKO

No comments:

Theme images by imagedepotpro. Powered by Blogger.